Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wadudu washambulia makazi ya wakimbizi Warohingya, IOM yachukua hatua.

 Wafanyakazi wa Rohingya wanatumia mianzi  kujenga daraja na mitaro katika kambi ya Kutupalong ,Bangladesh.
© UNHCR/Patrick Brown
Wafanyakazi wa Rohingya wanatumia mianzi kujenga daraja na mitaro katika kambi ya Kutupalong ,Bangladesh.

Wadudu washambulia makazi ya wakimbizi Warohingya, IOM yachukua hatua.

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la wahamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM kupitia taarifa iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi, limesema limeanza shughuli kubwa ya kuweka dawa katika miti ya mianzi inayotumika kujengea makazi ya dharura wakimbizi wa Rohingya walioko katika kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani, Cox’s Bazar nchini Bangladesh.

Wadudu wamekuwa wakishambulia miti hiyo kwa kiasi kikubwa kwenye nyumba zinazohifadhi takribani familia 240,000 na hivyo kuhitaji matengenezo makubwa yanayohitaji miti mipya ya mianzi.

Joel Millman, msemaji wa IOM amesema ili kusaidia kupambana na changamoto hiyo ya wadudu waharibifu, IOM imeanzisha kituo maalumu kusini mwa Cox’s Bazar ambacho kitapanuliwa zaidi katika wiki chache zijazo ili kiweze kumudu kushughulikia miti ya mianzi ipatayo 40,000 kwa mwezi, idadi inayotosha kuboresha makazi 6,000 hadi 7000.

Taarifa ya IOM imesema mti wa mwanzi ambao haujawekewa dawa unaweza kudumu kwa angalau miaka mitatu lakini kutokana na wadudu miti mingi imekuwa ikiharibika ndani ya kipindi cha miezi sita tu. Dawa itaifanya miti hii kudumu kwa miaka mingi zaidi.

Kwa mujibu wa maelezo ya Yoga Sofyar mtaalam anayefanya kazi na IOM katika mradi huu na ambaye pia amesaidia kutengeneza dawa ya kuhifadhi miti ya mianzi, dawa inayotumika ni ya asili na itakuwa ikichujwa na kutumika tena ili isiharibu mazingira. Vile vile takataka za mianzi zitakazosalia zitatumika kama mbolea katika mashamba ya karibu.

Takribani warohingya milioni moja hivi sasa wanaishi Cox’s Bazar katika makazi ambayo yamejengwa kwa dharura kwa kutumia miti ya mianzi katika vilima vya Bangladesh tangu walipoyakimbia machafuko nchini mwao Myanmar mwishoni mwa mwaka jana 2017.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.