Licha ya ofisi za CENI Kinshasa kutiwa moto, uchaguzi uko palepale- CENI

13 Disemba 2018

Moto mkubwa umeteketeza vifaa vya uchaguzi kwenye ofisi za tume huru ya taifa ya uchaguzi, CENI kwenye mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Kinshasa. 

Kwa mujibu wa Radio Okapi, ambayo ni ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO, moto huo ulianza leo asubuhi kwa saa za DR Congo kwenye moja ya bohari za tume hiyo ya taifa ya uchaguzi nchini humo.

CENI inasema kuwa vifaa vya uchaguzi vilivyochomwa moto ni vile ambavyo vilikuwa vinalenga wapiga kura wa mji mkuu Kinshasa kwenye uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika tarehe 23  mwezi huu wa Desemba.

Akihojiwa na radio Okapi, msemaji wa CENI Jean-Pierre Kalamba amesema kuwa,

“Kwa sasa tunaweza kuthibitisha tukio hilo la moto kwenye moja ya ofisi yetu asubuhi ya leo na tutatoa tathmini kamili baadaye. Na tunakadiria kwamba kile ambacho kimeteketezwa hakiwezi kusitisha mchakato wetu. Unafahamu kuwa katika bohari hiyo kuu kulikuwepo vifaa kwa ajili ya Kinshasa na pia magari ambayo yamechomwa. Kwa sasa tunajua hasara ni kubwa lakini tunashukuru Mungu kuwa vifaa vya uchaguzi kwa majimbo mengine 25 havikuwepo Kinshasa, vilishahamishiwa majimboni.”

Akizungumzia kitendo hicho, cha ofisi kutiwa moto, Felix Tshisekedi, mmoja wa wagombea wa kiti cha urais kupitia chama cha upinzani cha Democracy and Social Progress (UDPS) amelaani akidai kuwa hofu yake ni kwamba serikali ya DRC itahusisha moto huo na wapinzani wake.

"Serikali katu haiktana kufanya uchaguzi mzuri, wala haikutaka kuona uchaguzi huu unafanyika. Iweje eneo hili ambalo linapaswa kuwa moja ya maeneo yanayolindwa zaidi nchini wakati huu iungue hivi kwa urahisi?” amehoji Tshisekedi.

Tayari CENI imeahidi kufanyika kwa uchunguzi na kwamba uchaguzi  utafanyika kama ulivyopangwa

Moto huo kwenye ofisi za CENI mjini Kinshasa umetokea siku 10 baada ya kuanza kwa maandalizi ya uchaguzi huo wa rais na wabunge.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter