Hatimaye uchaguzi DRC kufanyika leo isipokuwa katika wilaya 5

30 Disemba 2018

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, wapiga kura wanachagua Rais, wabunge na magavana katika uchaguzi mkuu ambao wilaya tano nchini humo hazitapiga kura kutokana na sababu za ukosefu wa usalama na mlipuko wa Ebola.

Maeneo hayo ni Beni, Beni Mjini, Butembo Mjini katika jimbo la Kivu Kaskazini na mji wa Yumbi ulioko jimbo la Mai-ndombe ambapo sasa wapiga kura watatekeleza haki  yao hiyo ya kikatiba mwezi Machi mwakani ingawa matokeo ya urais yatatangazwa tarehe 15 Januari na Rais kuapishwa tarehe 18 mwezi huo huo wa Januari.

Akizungumzia uchaguzi huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake siku ya Ijumaa mjini New York, Marekani amewasihi mamlaka nchini DR Congo, viongozi wa kisiasa wa pande zote, tume ya uchaguzi CENI na jumuiya za kijamii kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha kunakuwa na mazingira yasiyo na vurugu kusudi siku ya uchaguzi wapiga kura wote wanaostahili waweze kupiga kura zao kwa amani.

Aidha Katibu Mkuu Guterres amewahimiza wananchi wa DRC kuitumia fursa hii ya kihistoria kushiriki katika kuimarisha taasisi za kidemokrasia za nchi yao.

Guterres amewakumbusha wadau wote wa uchaguzi huo kuwa wana jukumu muhimu la kufanya katika kuzuia vurugu za uchaguzi kwa kuepuka aina yoyote ya kuchochea na hali ya kukwamisha kwa maeno au matendo yao. Pia ametoa wito kwa kila mmoja kulinda na kuhakikisha ufikaji salama katika vituo vya afya katika maeneo yaliyoathirika na ebola.

Vilevile Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekumbushia ahadi ya Umoja wa Mataifa kusaidia makabidhiano ya madaraka kwa amani katika Jamhuri ya kidemkrasia ya Congo.

Mapema Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC Leila Zerrougui alielezea masikitiko yake kufuatia taarifa ya kwamba baadhi ya maeneo nchini humo hayataweza kushiriki kwenye uchaguzi huo hadi mwezi Machi mwakani.

Jumla ya wagombea 21 wanawania nafasi ya kiti cha urais ambapo mgombea mwanamke ni mmoja pekee.

Rais Joseph Kabila ambaye amekuwepo madarakani tangu mwezi Januari mwaka 2001 alikamilisha awamu zake mbili za uongozi miaka miwili iliyopita lakini amekuwepo madarakani kwa mujibu wa kipengele cha kusimamia mpito kuelekea uchaguzi mkuu ambao umekuwa ukiahirishwa tangu mwaka 2016.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter