CENI yamtangaza Tshisekedi rais mteule DRC, Guterres atoa kauli

9 Januari 2019

Tume ya huru ya taifa ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, CENI imemtangaza Felix Antoine Tshisekedi Tshilombo kutoka chama cha UDPS, kuwa mshindi wa kiti cha urais kufuatia uchaguzi uliofanyika nchini humo tarehe 30 mwezi uliopita wa Desemba.
 

Ukurasa wa mtandao wa Twitter wa CENI umeonyesha kuwa Tshisekedi amepata asilimia 38.57 ya kura zote zilizopigwa akifuatiwa na Martin Fayulu Madidi wa muungano wa vyama vya upinzani aliyepata asilimia  34.83 ilhali Emmanuel Ramazani kutoka chama tawala akipata asilimia 23.84.

Kufuatia matokeo hayo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema anatambua taarifa hizo na amepongeza wananchi wa DRC na wanasiasa kwa vile waliendesha na kushiriki uchaguzi huo wa rais, majimbo na wabunge kwa kutoa fursa jumuishi ya ushiriki.

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake mjini New York, Marekani jumatano usiku, Bwana Guterres ametoa wito kwa wadau wote kujiepusha na ghasia zozote na kuwasilisha malalamiko yoyote ya mchakato huo kwenye mifumo iliyowekwa kwa mujibu wa katiba ya DRC na sheria nyingine husika za uchaguzi.

Katibu Mkuu ameelezea matumaini yake kuwa CENI, mahakama ya katiba, serikali, vyama vya siasa na mashirika ya kiraia watawajibika katika kuimarisha utulivu na kuheshimu maadili ya kidemokrasia ya taifa hilo.

Halikadhalika amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea na ushirikiano na wadau wa kikanda na wale wa kimataifa katika kuimarisha amani, utulivu na maendeleo nchini DRC.

Hata hivyo wilaya tano nchini DRC hazikushiriki kwenye uchaguzi huu mkuu kutokana na sababu za kiusalama na ugonjwa wa ebola.

Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi iliyotolewa mwaka jana, Rais mteule anatarajiwa kuapishwa tarehe 18 mwezi huu wa Januari.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter