Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchaguzi mkuu DRC waahirishwa hadi Desemba 30 :CENI

Maandalizi ya ucahguzi huko DRC
MONUSCO/Alain Likota
Maandalizi ya ucahguzi huko DRC

Uchaguzi mkuu DRC waahirishwa hadi Desemba 30 :CENI

Haki za binadamu

Tume huru ya Taifa ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, CENI leo Alhamisi imetangaza mjini Kinshasa kuahirishwa kwa uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge uliokuwa umepangwa kufanyika tarehe 23 Desemba mwaka huu hadi tarehe 30 Desemba 2018.

Radio Okapi ambayo ni ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO imesema kuwa, Rais wa CENI Corneille Nangaa akithibitisha ripoti za kuahirishwa kwa uchaguzi huo amesema vikwazo vya kiufundi ndivyo vilivyofanya taasisi yake kushindwa kuendesha uchaguzi huu katika tarehe iliyotangaza.

Vikwazo hivyo ni pamoja na kuchelewa kuwasili kwa karatasi za kupigia kura milioni 3.5 ambazo zinapaswa kutumika katika vituo vya kupigia kura.

Amesema awamu ya mwisho ya makaratasi hayo yanayopaswa kupelekwa mji wa Kinshasa itawasili kutoka Korea ya Kusini jioni ya Jumamosi, Desemba 22.

 Asubuhi ya leo Bwana Nangaa alikuwa na mkutano wagombea wa urais   wa Jamhuri, uliotanguliwa na mkutano wa pande tatu wa CENI, Kamati ya kitaifa ya kufuatilia makubaliano, CNSA na serikali.

Waziri Mkuu Bruno Tshibala, Rais wa CNSA Joseph Olenga Nkoy na rais wa CENI Corneille Nangaa walishiriki katika mkutano huo wa pande tatu.