Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni muhimu kwa Afrika kujitosa katika biashara:UNCTAD

Biashara kama hii ya mjasiriamali huko Zambia anayebadili Chupa ambazo awali zilikuwa taka na kuzifanya mapambo zinaweza kupata wateja duniani kote kutokana na soko la mtandaoni.
UNIC Dar es salaam/Stella Vuzo
Biashara kama hii ya mjasiriamali huko Zambia anayebadili Chupa ambazo awali zilikuwa taka na kuzifanya mapambo zinaweza kupata wateja duniani kote kutokana na soko la mtandaoni.

Ni muhimu kwa Afrika kujitosa katika biashara:UNCTAD

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Biashara mtandaoni ambayo inaendelea kushika kasi sio tu katika mataifa yaliyoendelea bali pia katika nchi zinazoendelea ni chachu katika kukuza uchumi, kutoa ajira na kusongesha ajenda ya maendeleo endelevu au SDGs.

Hayo ni kwa mujibu wa Bernad Dadi, mkurugenzi wa kitaifa wa mifumo ya malipo katika benki Kuu ya Tanzania, ambaye yuko Nairobi nchini Kenuya akihudhuria mkutano wa wiki ya biashara mtandaoni barani Afrika.

Bwana. Dadi amesema kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi nyingi duniani hutegemea biashara

"Ukiangalia uchumi, sana hutegemea biashara. Kwa hiyo kwa kutumia elektroniki tutaweza kuharakisha biashara ifike kiuharaka kwa ueledi zaidi na hivyo mapato zaidi ya kuendeleza maendeleo ya wananchi"

Na kuhusu umuhimu wa mkutano huo kwa Afrika amesema

"Ni muhimu sana kwasababu inaleta wanachama kutoka hizi nchi mbalimbali kukaa pamoja kubadilishana mawazo na ni wapi tuendeleze zaidi na kipi kinahitaji kufanyiwa kazi zaidi, ni kipi kitahitaji nchi kushirikiana katika kutatua kama kuna tatizo au siyo tatizo hasa ukiangalia dunia inakoelekea katika njia za kufanya malipo za kielektroniki itatusaidia sana. Kenya, Tanzania na nchi nyingine kukaa pamoja kubadilishana mawazo kuona ni jinsi gani tunaweza kuendeleza biashara hizi kwa kutumia njia za kielekroniki"

Mkutano huo ulioandaliwa na kamati ya umoja wa Mataifa ya maendeleo na biashara UNCTAD, Muungano wa Afrika na muungano wa Ulaya umewaleta pamoja wawakilishi wa nchi na serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia na mashirika ya kimataifa kwa lengo la kubaini njia bunifu kwa ajili ya kulisongesha mbele bara la Afrika katika zama za uchumi wa kidijitali.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.