Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauritius yaibuka kidedea biashara mtandaoni Afrika.

Watu wanaumia mitandao kuagiza na kulipia bidhaa kote duniani.
ITU/G. Anderson
Watu wanaumia mitandao kuagiza na kulipia bidhaa kote duniani.

Mauritius yaibuka kidedea biashara mtandaoni Afrika.

Ukuaji wa Kiuchumi

Mauritius imechukua nafasi ya juu kwa nchi za bara Afrika zenye utayari wa kufanya biashara kwa njia ya mitandao.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya Kamati ya Umoja wa Mataifa ya biashara na maendeleo, UNCTAD mwaka ya mwaka 2018 kuhusu biashara mtandaoni iliyotolewa hii leo mjini Nairobi Kenya.

Kati ya nchi 43 za Afrika zilizojumuishwa miongoni mwa 151, 9 zimeshika nafasi za mwisho isipokuwa Mauritius ambayo imechukua nafasi ya 55 duniani, nafasi tatu za juu zikichukuliwa na Uholanzi, Singapore na Uswisi.

Katibu Mkuu wa UNCTAD, Dkt. Mukhisa Kituyi amesema, “Afrika inajikongoja nyuma ya maeneo mengine ya dunia katika utayari wa kutumia na kufaidika na uchumi wa kidijitali. Robo tatu ya watu wa barani Afrika bado hawajaanza kutumia intaneti.”

Hata hivyo Dkt. Kitui ameongeza kusema kuwa bara la Afrika linaonesha maendeleo katika viashiria vya biashara mtandaoni akisema tangu mwaka 2014 nchi za kusini mwa jangwa la Sahara zimepita tatu kati ya viashiria vinne vilivyotumika katika ripoti.

 “Tunakadiria kuwa kulikuwa na angalau wanunuzi wa mtandaoni wapatao milioni 21 barani Afrika kwa mwaka jana, pungufu ya asilimia 2 ya jumla ya dunia, nchi tatu yaani Nigeria, Afrika Kusini na Kenya zikichukua takribani nusu. Hata hivyo idadi ya wanunuzi wa mtandaoni barani Afrika imepanda kwa mwaka kwa asilimia 18 tangu 2014, kasi zaidi ya ile ya wastani wa kidunia wa asilimia 12” amesema Katibu mkuu wa UNCTAD.

Nchi tatu za juu za Afrika katika ripoti, kila moja ina ubora wake katika moja ya maeneo manne yaliyopimwa katika ripoti ambayo siyo tu inaangalia wanunuzi wa mtandaoni bali vitu vingine kama wepesi wa kulipa na kufikisha mzigo kwa mnunuzi.

Mauritius imeizidi kwa pointi 12 Nigeria ambayo ndiyo nchi ya Afrika inayoifuata kwa sababu Mauritius ina asilimia 90 ya wananchi wake wanaotumia benki au akaunti za fedha katika simu.

Nigeria ambayo ndiyo nchi yenye watu wengi zaidi barani Afrika imechukua nafasi ya pili kutokana na ubora wake katika masuala ya posta na Afrika kusini ikachukua nafasi ya tatu ikiwa na nchi nyingine za Afrika kama Cabo Verde, Gabon na Morocco kutokana na usambazaji wa intaneti ambapo inasemwa kuwa kati ya watu kumi, sita wanatumia mtandao huo. Afrika kusini inazizidi kiasi nchi nyingine kwa kuwa na uhakika wa intaneti.