Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mamia wakielekea Marrakech, CO24 nayo yajadili tabianchi na uhamiaji

Kimbunga Hagupit kilipopiga Ufilipino tarehe 5-6 Desemba 2014, hali ilikuwa mbaya kwani nchi  hiyo bado ilikuwa haijasahau madhara ya kimbunga Haiyan kilichotokea Novemba 2013.
OCHA/Jennifer Bose
Kimbunga Hagupit kilipopiga Ufilipino tarehe 5-6 Desemba 2014, hali ilikuwa mbaya kwani nchi hiyo bado ilikuwa haijasahau madhara ya kimbunga Haiyan kilichotokea Novemba 2013.

Mamia wakielekea Marrakech, CO24 nayo yajadili tabianchi na uhamiaji

Tabianchi na mazingira

Wakati mamia ya watunga sera wakikusanyika huko Marrakech nchini Morocco kwa ajili ya kukubaliana juu ya mkataba mpya wa kimataifa kuhusu uhamiaji, mkutano wa 24 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP24 huko Katowice Poland, nao unajikita katika njia thabiti za kusaidia nchi kukabiliana na ukimbizi wa ndani  utokanao na madhara ya mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ukosefu wa maji, mafuriko, vimbunga na kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari

 

Koko Warner ambaye anaongoza masuala ya uhamiaji kwenye sekretarieti ya mkataba wa mabadiliko  ya tabianchi, UNFCCC amesema, “mabadiliko ya hali ya hewa, mafuriko, ukame katika maeneo mengi, vimetishia usalama na njia za watu kujipatia kipato.”

Ingawa bado kuna changamoto katika kupata idadi kamili ya watu waliojikuta wakimbizi kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Umoja wa Mataifa unakisia kuwa zaidi ya watu milioni 258 wanaishi nje ya nchi zao za asili. Ongezeko la joto nalo linatarajiwa kuongeza idadi hiyo na kusababisha baadhi ya maeneo ya dunia yasiweze kuwa mahali salama kwa binadamu kuishi.

UN News Kiswahili
Mabadiliko ya tabianchi ni kweli

 “Mfano, iwapo wewe ni mkulima na mvua hainyeshi kwa miaka kadhaa mfululizo, ghafla unaweza kupoteza siyo tu njia yako ya kujipatia chakula, bali pia njia ya kujipatia kipato na usawi wa familia  yako utakuwa mashakani,” amefafanua Bi. Warner akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa huko Katowise.

Hivi sasa, uwezekano wa mtu kukimbia makazi  yake kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi ni mara nne zaidi kuliko anavyoweza kukimbia kwa sababu ya vita au mizozo.

MAPENDEKEZO YA KUSAIDIA NCHI KUKABILI UKIMBIZI UTOKANAO NA MABADILIKO YA TABIANCHI

Ili kupatia suluhu hali hiyo ,tayari kuna mapendekezo lukuki ya kusaidia nchi kukabiliana na ukimbizi usababishwao na athari za mabadiliko ya tabianchi, mapendekezo ambayo yamewasilishwa kwenye mkutano wa COP24.

 “Tumetoka mbali. Ukimbizi utokanao na mabadiliko ya tabianchi haukuwepo au haukupatiwa kipaumbele sana wakati wa mahadiliajo hadi mwaka 2010 huko Cancún.Huko Paris, miaka mitano baadaye, serikali ziliomba mapendekezo ya jinsi gani zinaweza kujiandaa na kukabilia hali hiyo, na sasa hapa Katowice, tunatarajia kuyapitisha,” amesema Bi. Warner.

Mapendekezo hayo yaliyowasilishwa mbele ya nchi 197 wanachama wa UNFCCC ni pamoja na mipango tangulizi dhidi ya hali inayoweza kutokea, mashauriano na uchambuzi wa data na ushirikiano baina ya mataifa.

Nyaraka hiyo ya mapendekezo iliandaliwa na kikosi kazi cha masuala ya ukimbizi wa ndani na imewasilishwa leo ikisubiri kupitishwa na wataalamu kutoka nchi wanachama, ikifuatiwa na kupitishwa na wajumbe kutoka ngazi ya nchi wizara.

 “Lengo hasa ni kusaidia nchi kuelewa kiwango cha kile kinachoweza kutokea na hivyo kujiandaa kukabiliana nayo. Ni jinsi ya kusaka mbinu za kupunguza machungu na kuhakikisha usalama na utu wa watu walio hatarini kufurushwa pindi majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi yanapotokea,” amesema Bi. Warner.

Majadiliano haya yafanyika kuelekea kupitishwa kwa mkataba mpya kuhusu uhamiaji jumanne ijayo huko Marrakech.