Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rasimu ya azimio la Marekani dhidi ya Hamas yagonga mwamba Baraza Kuu

Mkutano wa 47 wa kikao cha 73 cha baraza kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu mashariki ya Kati.
UN Photo/Loey Felipe
Mkutano wa 47 wa kikao cha 73 cha baraza kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu mashariki ya Kati.

Rasimu ya azimio la Marekani dhidi ya Hamas yagonga mwamba Baraza Kuu

Amani na Usalama

Rasimu ya azimio lililowasilishwa na Marekani dhidi ya kundi la Hamas kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa imegonga mwamba hii leo baada ya kutopata kura za kutosha kutoka kwa wajumbe. Rasimu hiyo iliyojadiliwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani ni ya kulikosoa  kundi la Hamas kwa  kuvurumisha maroketi hadi Israel kutokea Ukanda wa Gaza. 

Rasimu hiyo inalaani vikali vitendo vya kundi la Hamas vya kurusha maroketi kila mara kuelekea Israel, ikisema “kunachochea ghasia na pia kuhatarisha maisha ya raia wa kawaida.” Rasimu ilitaka kundi la Hamas na makundi mengine yenye silaha, likiwemo kundi la Kipalestina la Islamic Jihad, kuacha uchokozi na visa vya kutumia mabavu ikiwemo kutumia vifaa kama tiara vyenye kubeba vilipuzi. Pia  rasimu hiyo  inalaani hatua ya Hamas mjini Gaza ya kujenga miundombinu ya kijeshi mfano  njia za kupitia chini ya ardhi na kuzitumia kuingia kinyemela ndani ya Israel.

Isitoshe kundi la Hamas linalaumiwa kwa kuweka mizinga katika maeneo ya raia. Rasimu inasema raslimali zinazotumiwa na Hamas kufanya hayo zingetumiwa  kushughulikia mahitaji muhimu na  ya haraka ya raia wa Gaza.

Baada ya kupitia rasimu hiyo balozi wa Marekani, Nicky Healy, aliomba kuipigia kura, lakini ukazuka mvutano kuhusu akidi ya kura hiyo kuweza kupitishwa. Huku Marekani ilikuwa inataka kiwango cha kutosha cha kura kuweza kuipitisha lakini balozi wa Kuwait, Al-Otaibi, kwa niaba ya kundi la mataifa ya kiarabu  akapendekeza  theluthi mbili ndiyo ichukuliwe na kusema kuwa nchi zao, yaani Saudi Arabia, Bahrain, Falme za Kiarabu  na Yemen zitaipigia kura ya hapana rasimu hiyo.

Hivyo pendekezo la theluthi mbili ya kura likapitishwa kwa kura 86 za ndiyo na 57 za hapana na nchi 33 hazikupiga kura.