Wimbi kubwa la wagonjwa ni shinikizo kwa hospitali ya wakimbizi ya Maban Sudan kusini:UNHCR
Hospitali ya wakimbizi ya Maaban iliyoko jimbo la Bunj nchini Sudan Kusini iko katika shinikizo kubwa baada ya kuzidiwa na wimbi la wagonjwa huku vifaa, wauguzi na dawa vikiendelea kuwa haba.
Hospitali hiyo inayoendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR inahudumia zaidi ya wakimbizi 140,000 wengi wakiwa ni kutoka Sudan na jamii zinazowahifadhi . Dkt. Evan Atar Adaha mganga mkuu na daktarin bingwa wa upasuaji katika hospitali hiyo ya rufaa anaeleza sababu
“Watu ambao walikuwa hawaji hapa kabla ya mkataba wa amani uliotiwa saini hivi karibuni na ambao walikuwa wametengwa wakiogopa kurudi katika eno hili, sasa kufuatia tangazo la amani wameanza kurejea kutoka maeneo yote hayo na wanakuja hospital, hatuwezi kumrudisha mgonjwa , lakini sasa inatuathiri sana kuanzia rasilimali watu, madawa na vifaa vya tiba na hatuwezi kukabiliana na hali hii.”
Ameongeza kuwa wanachohitaji haraka kwa hivi sasa ni wahudumu wa afya, madawa na vifaa muhimu ili kuweza kutoa huduma ifaayo kwa maelfu ya wagonjwa ambao wengine wanatoka mbali zaidi katika maeneo ya Renk na Melut ambako vituo vya afya vilisambaratishwa wakati wa vita vya mwaka 2013.
Dkt. Evan Atar Adaha ambaye ni daktari pekee wa upasuaji katika hospitali hiyo ya Maban, kwa kutambua mchango wake katika kuokoa maisha ya wakimbizi mwezi Septemba mwaka huu alitunukiwa tuzo ya kifahari ya wakimbizi ya Nansen inayotolewa kila mwaka na shirika la UNHCR.