Chonde chonde lindeni haki za wahudumu wa kibinadamu Sudan Kusini- UNHCR

3 Disemba 2019

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, limetaka ulinzi zaidi kwa wafanyakazi wa kutoa misaada nchini Sudan  Kusini kufuatia shambulizi la mwishoni mwa wiki lililofanywa na watu wenye silaha dhidi ya wafanyakazi wa kimataifa wa kusambaza misaada.

Shambulio hilo baya limefanyika asubuhi ya Jumapili ya tarehe Mosi mwezi huu wa Desemba ambapo watu wenye silaha walivamia jengo la shirika la kiraia mjini Bunj, kwenye kaunti ya Maban jimboni Upper Nile na kushambulia wafanyakazi huku wakipora mali zao.

Taarifa ya UNHCR imelaani vikali shambulio hilo dhidi ya wafanyakazi hao ambao limesema walikuwa wanajitolea ili kuboresha maisha ya wakimbizi wa ndani na raia wa Sudan Kusini walio kwenye taabu.

Katika miezi michache iliyopita, kumekuwepo na ongezeko la mashambulizi dhidi ya wahudumu wa kibinadamu nchini Sudan Kusini ambapo ghasia ya Jumapili imetokea mwezi mmoja tu tangu wafanyakazi watatu wa Umoja wa Mataifa wauawe kwenye eneo la Equatoria ya Kati nchini Sudan Kusini.

“Usalama wa wahudumu wa kibinadamu umesalia changamoto kubwa katika taifa hilo changa zaidi duniani, hali ambayo inakwamisha usambazaji wa misaada ya kibinadamu,” imesema UNHCR huku ikitaka kuheshimiwa zaidi kwa sheria za kibinadamu na za haki za binadamu za kimataifa za kulinda raia na wahudumu wa kibinadamu dhidi ya ghasia na kwamba watekelezaji wafikishwe mbele ya sheria.

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud