Mchango wa wanawake ni bayana katika tamko la haki za binadamu-Bachelet

5 Disemba 2018

“Katika siku tano zijazo, kama mjuavyo tutaadhimisha miaka sabini ya nyaraka ya aina yake ambayo ni tamko la haki za binadamu za Umoja wa Mataifa.” Hivyo ndivyo ilivyoanza hotuba yake Kamishna Mkuu wa Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, Michele Bachelet

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, hii leo Kamishna Mkuu huyo amesema anaamini kwamba tamko hilo ni muhimu leo kama ilivyokuwa miaka sabini iliyopita.

 Bi. Bachelet amesema katika miongo kadhaa tamko hilo limetoka kuwa  makubaliano tu na kuwa nyenzo muhimu  ya viwango ambavyo vimetamalaki katika kila sheria ya kimataifa.

Ameongeza kuwa mapendekezo yake ni muhmu na yanaweza kutumika katika kututatua changamoto za sasa na kwamba yanalenga haki za makundi ya watu tofauti duniani kwa mfano haki za wapenzi wa jinsia moja au wale waliobadili jinsia, LGBTI ambao wachache wangethubutu kutaja au kuweka bayana hilo katika miaka ya 1948.

Bi Bachelet amesema suala la jinsia limezingatiwa katika kila kipengee, na halikuanza leo wala jana tangu zama hizo na mara mbili ambapo kunaashiriwa mwanamume na familia yake, huku nyaraka nzima ikitumia maneno, “kila mtu” au “wote” katika ibara zote 30 bila kulenga jinsia moja.

 Kamishna Mkuu huyo ameongeza kuwa matumizi hayo yanaweka bayana kwamba  kwa mara ya kwanza katika historia ya uundaji sheria za kimataifa, wanawake walikuwa na mchango mkubwa katika kuandika tamko hilo la haki za binadamu akisema..

 “Mchango wa Eleanor Roosevelt, ambaye alikuwa mwenyekiti wa kamati ya waandaaji unajulikana. Kisichojulikana ni ukweli kwamba wanawake kutoka Denmark, Pakistan na nchi za kikomunisti na nchi nyingine walikuwa na mchango muhimu.”

 Amesisitiza kuwa mchango muhimu wa Hansa Mehta kutoka India ulihakikisha sentensi ya kifaransa, “wanaume wote wamezaliwa sawa na huru" inabadilishwa na kuwa “watu wote wamezaliwa sawa na huru”

Bi Bachelet amesema tamko hilo ni la kawaida lakini la mabadiliko ukizingatia haki za wanawake na makundi ya walio wachache.

 “Hansa Mehta alikataa kauli ya Eleanor Roosevelt ya kusema neno wanaume itaeleweka kama ni kujumuisha pia wanawake-kauli iliyokubalika wakati huo. Alisisitiza kuwa nchi huenda zikatumia maneno hayo kudhibiti haki za wanawake badala ya kuziimarisha. Ninaamini alikuwa sahihi.”

 Kamishna Mkuu huyo amehimiza umuhimu wa kila mtu kusimama kidete kwa ajili ya haki zilizoorodheshwa na tamko kwa kila mtu na sio sisi tu lakini kwa ajili ya kila binadamu, haki ambazo ziko katika hatari ya kukiukwa kwa ajili ya kusahau kwetu na kwa viongozi wetu au kwa ajili ya kuzipuuza.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter