Chondechonde DRC tendeni haki katika kuelekea uchaguzi mkuu:Bachelet

5 Disemba 2018

Kamishina Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu Michele Bachelet ameisihi serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kuhakikisha inatekeleza haki za binadamu hasa wakati huu ambapo taifa hilo l inajiandaa kwa uchaguzi mkuu.

Bi. Bachelet amesema wameshuhudia na kuendelea kupokea  taarifa za ongezeko la ukiukwaji wa haki za binadamu wakati huu taifa hilo likijiandaa na uchaguzi na hivyo wanazichagiza pande zote husika ikiwemo serikali na upinzani kutekeleza ahadi waliyoiweka katika makubaliano ya Disemba 2016 ambayo ni,“kuwaachilia huru wafungwa wote wa kisiasa , uwajibikaji wa ukiukaji wa haki za binadamu na  kukomesha matumizi ya nguvu kupita kiasi ya polisi au vikosi vya usalama wakati wa maandamano.”

Ameongeza kuwa machafuko zaidi wakati huu itakuwa ni zahma kubwa kwa taifa ambalo tayari lina mzigo wa vita na mlipuko wa Ebola ,"Tumeshuhudia pia kuendelea kwa mapigano katika sehemu za DRC katika Kivu ya Kaskazini nah ii inamaanisha kwamba machafuko yanayosababishwa na baadhi ya makundi yenye silaha yamesababisha kundi kubwa la watu kutawanywa.”

Amewataka pia wananchi kuonyesha msikamano na mchango wao katika juhudi za kudumisha amani na utulivu katika kipindi hiki ambacho ni muhimu kwa demokrasia ya taifa hilio lililoghubikwa na vita kwa miongo mingi na kufanya mamilioni ya watu wake kuwa wakimbizi wa ndani na nje.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter