Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utamaduni haupaswi kuwa kisingizio cha kubinya haki zingine

Wasimamizi wa uchaguzi wahesabu kura wakati wa uchaguzi wa bunge la chini Baidoa, Somalia Novemba 2016.
UN Photo/ Sabir Olad
Wasimamizi wa uchaguzi wahesabu kura wakati wa uchaguzi wa bunge la chini Baidoa, Somalia Novemba 2016.

Utamaduni haupaswi kuwa kisingizio cha kubinya haki zingine

Haki za binadamu

Mila na desturi za kitamaduni zina mchango mkubwa katika jamii endapo zitaenziwa kwa kuheshimu haki zingine za binadamu. Hata hivyo wakati mwingine jamii hutumia haki za kitamaduni kama kisingizio cha kukandamiza wengine au kubinya haki zingine za binadamu katika jamii. 

Wakati huu ambako tamko la haki za binadamu likielekea kutimiza miaka 70, Umoja huo unahimiza jamii na mataifa yote duniani kutumia haki za kuenzi mila na utamaduni kama ilivyoainisha katika ibara 22 ya tamko hilo isemayo “kila mtu, kama sehemu ya jamii, ana haki ya ulinzi wa jamii pamoja na haki ya kutambua, kupitia juhudi za kitaifa kujiendeleza, hivyo ana haki ya kiuchumi na kitamaduni,” kuzingatia haki hizo kwa kuleta maendeleo na sio kuyakwamisha.

Somalia  taifa lililoghubikwa na vita kwa zaidi ya miongo miwili utamaduni wake uliokita mizizi wa kuendesha kila kitu kwa misingi ya koo mbali ya kusaidia kwa upande mmoja unabinya haki zingine kama anavyofafanua mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Somlia , Bahame Tom Nyanduga alipozungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa mataifa, “ Kuwepo na mfumo huo, umeminya sana haki za wanawake na jitihada ipo sasa hivi ya kuhakikisha kwamba wanavyorudi katika mfumo wa katiba ya  kudumu  angalau changamoto za kuwepo kwa mfumo huo wa kimila uweze kuangaliwa yale ambayo ni matokeo hasi kwa kweli yaweze kutolewa kwenye mfumo wa utawala.”

Na kwa mazuri je ? Bw Nyanduga ameongeza," Mfumo wa mila na koo unaosimamiwa na zile koo ulisaidia sana kuweka jamii ya Somalia pamoja katika kipindi ambako kulikuwa na ombwe la utawala wa serikali. Na hilo limewasaidia kujikusanya ndio wakarudi kuunda serikali mwaka 2012. "