Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ILO yaleta matumaini kwa watu wenye ulemavu Jordan

Stadi kwa wakimbizi wa Syria ni muarobaini wa kuboresha maisha yao.
UNICEF/UN0201091/Herwig
Stadi kwa wakimbizi wa Syria ni muarobaini wa kuboresha maisha yao.

ILO yaleta matumaini kwa watu wenye ulemavu Jordan

Wahamiaji na Wakimbizi

Nchini Jordan mradi wa shirika la kazi duniani ILO wa kujenga stadi za kutengeneza picha umeleta matumaini sio tu kwa wenyeji bali pia kwa wakimbizi wa Syria. Taarifa zaidi na John Kibego.

Ndani  ya chumba kimoja cha mafunzo, wanawake kwa waume, wenye ulemavu na wasio na ulemavu wamejumuika pamoja kupata mafunzo ya kutengeneza picha zitokanazo na kubandika vipande vidogo vidogo vya chupa, mawe au mbegu katika vitambaa au vibao.

Mafunzo yanaendeshwa kwa ushirikiano kati ya ILO na taasisi ya Sanaa ya Madaba nchini Jordan ikipatia mafunzo wanafunzi 61, idadi kubwa ni watu wenye ulemavu kutoka jamii ya wenyeji Jordan na wakimbizi wa Syria.

Wanafunzi wako makini sana na miongoni mwao ni Rahma Khairallah, raia wa Jordan ambaye anabandika chupa kwenye kitambaa kwa kutumia mguu. Rahma anasema kuwa “Walinieleza, nikaogopa kushiriki. Lakini baadaye nikafikiria bora nijilazimishe nishiriki mafunzo haya yanaweza kunipatia fursa.” 

Maha Kattah ambaye ni mratibu wa mafunzo haya kutoka ILO anasema lengo ni kuhakikisha hatimaye washiriki wanaweza kujipatia kipato kupitia stadi hizi.

Washiriki wanasaidiana wengine wakikata vipande vya chupa wengine wakibandika huku wengine wakichora maua au picha za kubandikia vipande hivyo .

Rahma anafunguka ya kwamba  "Nimependa sana haya mafunzo. Ni matumaini yangu kuwa yataniwezesha kupata kazi ili nami niweze kuwa na maisha yenye furaha na utu. Napenda kuwaeleza wengine wasikubali ulemavu wa viungo usiingilie maisha yao. Watoke nje na waonyeshe ulimwengu kuwa wanaweza kufanya kazi ”