Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila sekunde 24 mtu 1 hupoteza maisha katika ajali barabarani:Guterres 

Huduma za dharura baada ya ajali kutokea katika moja ya maeneo ya mji wa New  York, nchini Marekani. Huduma za haraka huokoa maisha lakini pia UN inataka hatua madhubuti kuzuia ajali hizo.
UN News/Vibhu Mishra
Huduma za dharura baada ya ajali kutokea katika moja ya maeneo ya mji wa New York, nchini Marekani. Huduma za haraka huokoa maisha lakini pia UN inataka hatua madhubuti kuzuia ajali hizo.

Kila sekunde 24 mtu 1 hupoteza maisha katika ajali barabarani:Guterres 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Hatua za haraka zinahitajika na kusalia kuwa za muhimu sana katika kuokoa maisha ya maelfu na maelfu ya watu yanayopotea kila siku katika ajali za barabarani. Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe maalum wa kuadhimisha siku ya kimataifa ya usalama barabarani ambayo kila mwaka huadhimishwa Novemba 17. “Natoa wito kwa kila mtu kujiunga nasi katika kushughulikia changamoto ya kimataifa ya janga la usalama barabarani.”

Guterres amesema ajali za barabarani ni chanzo kikubwa cha vifo miongoni mwa watoto na vijana wa umri wa kuanzia miaka 5-29. Ameongeza kuwa hatari ya kufa kutokana na ajali za barabarani iko juu mara tatu zaidi katika nchi za kipato cha chini kuliko katika nchi za kipato cha juu.

Katibu mkuu amesema “zaidi ya nusu ya vifo vyote vya ajali za barabarani ni miongoni mwa makundi yaliyo hatarini ya watumiaji wa barabara kama watembea kwa miguu, waendesha baiskeli na waendesha pikipiki ambao kwa pamoja wanajulikana kama watumiaji walio hatarini”.

Guterres amesema watumiaji hao wa barabara walio hatarini ni nusu ya watu wote wanaokufa katika ajali za barabarani kote duniani. Na kiwango kikubwa cha watu hao kupoteza maisha katika nchi za kipato cha chini kuliko zile za kipato cha juu.

Tangu kupitishwa Siku ya kuwakumbuka waathirika wa ajali za barabarani duniani, maadhimisho hayo yamesambaa katika nchi nyingi duniani na katika kila bara. Ujumbe wa Katibu Mkuu unasema siku hiyo imekuwa nyenzo muhimu sana katika juhudi za kimataifa za kupunguza vifo na majeruhi wa ajali za barabarani.

Pia umesema siku hiyo ni fursa ya kuweka msukumo katika kiwango cha athari za kiuchumi na kihisia zinazosababishwa na ajali za barabarani na kutambua machungu na madhila yanayowakabili waathirika wa ajali za barabarani na kazi kubwa ya msaada na huduma za uokozi.

Maisha sio sehemu ya vipuri vya gari

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa kaulimbiu mwaka huu imejikita katika masuala matatu ya mpango wa kimataifa kwa ajili ya muongo wa kuchukua hatua kwa ajili ya usalama barabarani na magari salama sambamba na juhudi za kimataifa, aina ya uwezo wa barabara ambao uko mahali pote ulimwenguni lakini bado unasababisha idadi kubwa ya vifo, majeraha makubwa na magonjwa kila mwaka, vyote vikiwa ni athari za ajali za barabarani na kupitia uchafuzi wa hewa.

TAGS: Ajali za barabarani, vifo, waendesha baiskeli, watembea kwa miguu, waendesha pikipiki, Siku za UN