Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machafuko mashariki ya Syria yasababisha vifo vya watoto 30-UNICEF

Watoto wa Syria wakiwa katika kambi za wakimbizi. Ni miongoni mwa waathirika wakubwa  wa vita vya Syria.
© UNICEF/Aaref Watad
Watoto wa Syria wakiwa katika kambi za wakimbizi. Ni miongoni mwa waathirika wakubwa wa vita vya Syria.

Machafuko mashariki ya Syria yasababisha vifo vya watoto 30-UNICEF

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema lina wasiwasi mkubwa kufuatia ripoti za hivi karibuni za kuuawa kwa watoto wapatao 30 wakati wa mapigano yaliyotokea kijiji cha Al Shafa mashariki mwa Syria.

Mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati Geert Cappelaere amesema mauaji haya yaliyoripotiwa yanadhihirisha kuwa vita dhidi ya watoto nchini Syria bado havijakoma.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo huko Damascus Syria na Amman Jordan, Bwana Cappelaere amesema “kwa takribani miaka nane ya vita sasa, kanuni za kimsingi za kulinda watoto zimepuuzwa huku kukiwepo na matokeo mabaya dhidi ya watoto nchini Syria.”

Ametoa mfano akisema kuwa “kati ya mwezi Januari na Septemba mwaka 2018, Umoja wa Mataifa umethibitisha mauaji ya watoto 870- idadi ambayo ni ya juu zaidi katika miezi tisa ya mwanzo ya mwaka tangu vita hivyo vya Syria vianze mwaka 2011. Hivi ni visa tu vilivyothibitishwa ambapo idadi halisi inaweza kuwa kubwa zaidi.”

Mkurugenzi huyo wa UNICEF kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini ametoa wito kwa pande zote kinzani  nchini Syria zilinde watoto bila kujali eneo walilopo nchini Syria na ni nani anamiliki eneo hilo.