Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Namkumbusha mama anawe mikono kabla ya kupika- Nenga

Muhamasishaji akiwafundisha watoto kuhusu mbinu sahihi za unawaji mikono, ili kuzuia kuenea kwa magonjwa, ikiwa ni pamoja na Ebola. Picha: UNICEF / Timothy La Rose

Namkumbusha mama anawe mikono kabla ya kupika- Nenga

Afya

Jumuiya ya kimataifa na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wanaimarisha juhudi za kudhibiti mlipuko wa Ebola kwenye jimbo la Equateur nchini humo.     

Utoaji wa chanjo dhidi ya Ebola unaendelea katika mji Mbandaka ikiwa ni siku ya pili, huku ikiripotiwa pia kuanza kwa utoaji wa chanjo huko Bikoro ambako ndiko mlipuko ulianzia.

Katika kituo cha afya cha Mbandaka ambako ndiko kuna kituo cha kutibu Ebola, tayari watoa huduma ya afya wamepatiwa chanjo hiyo.

Mkurugenzi wa kituo hicho Dkt. Manzibe Hilaire amesema, “ ni lazima kwanza tujilinde wenyewe. Kila mtu anayefika kituo hiki lazima kwanza anawe mikono kama njia ya kujikinga.” 

"ni lazima kwanza tujilinde wenyewe. Kila mtu anayefika kituo hiki lazima kwanza anawe mikono kama njia ya kujikinga.”

Pamoja na utoaji wa chanjo, wahudumu wa afya wanaendesha kampeni za kuhamasisha jamii kuelewa kuhusu ugonjwa wa Ebola ili waweze kujikinga dhidi yake.

Wanafunzi wa shule nao wananawa mikono kwa maji yenye dawa maalum na hufanya hivyo kabla ya kuingia darasani na kabla ya kula.

Nenga Myongo, mwanafunzi wa miaka 10 anasema, “tunalazimika kufanya hivi. Na badala ya kusalimiana kwa kushikana mikono, tunapungiana na hatupaswi kukaribiana.”

 Mwanafunzi huyo anadhihirisha jinsi kampeni ilivyoshika kasi kwa kuwa anaongeza kuwa hata nyumbani, mama yake kabla ya kupika chakula ni lazima anawe mikono na akisahau, anamkumbusha.

Nenga anasema anafanya hivyo pia kwa baba yake na kaka yake.

Shirika la afya ulimwenguni, WHO linasema zaidi ya chanjo 7,500 za kukinga ugonjwa huo wa Ebola zimepelekwa DRC.

Tangu kuibuka kwa Ebola tarehe 8 mwezi huu wa Mei huko DRC, watu 27 wamefariki dunia na wengine 58 wameshukiwa kuwa na ugonjwa huo.

Wagonjwa wengi wamepatikana katika mji wa Bikoro ulioko maeneo ya mashambani ilihali wagonjwa wane waliripotiwa mjini Mbandaka, mji wenye watu zaidi ya milioni 1.