Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Juhudi dhidi ya Ebola DRC zijumuishe watoto- UNICEF

UNMEER ni Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kukabiliana na dharura ya Ebola, uliomaliza majukumu yake mwezi uliopita. Picha ya UNMEER/ akaunti ya Twitter.

Juhudi dhidi ya Ebola DRC zijumuishe watoto- UNICEF

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limetaka harakati za kukabiliana na mlipuko wa Ebola huko Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC ujumuishe watoto.

Mwakilishi wa UNICEF huko DRC Dkt. Gianfranco Rotigliano amesema hiyo ni muhimu kwa kuwa watoto wataendelea kuwa hatarini kuambukizwa ugonjwa wa ebola, endapo nguvu haitaelekezwa kuwajumuisha katika mikakati ya kuzuia mambukizi ya mlipuko huo ..

Dkt. Rotigliano amesema  shule ni pahala pazuri kwa ajili ya kuwahimiza na kuwaelimisha watoto kuhusu hatua na tahadhari dhidi ya maambukizi ya Ebodla ikiwa ni pamoja na kunawa mikono kila wakati na pia kuwapima joto mwilini ili kubaini kama wana dalili za homa au la.

UNICEF  tayari imeongeza juhudi za kuzuia  maambukizi katika baadhi ya shule na maeneo ya vituo vya afya.

Hii inajumuisha jitihada zinazoendelea za kuwa na maeneo ya kunawa mikono katika shule 277 na kusaidia shughuli za kuhamasisha na kuwafikia zaidi ya watoto  13,000 Mbandaka, Bikoro na Iboko katika jimbo la Equateur.

Shirika hilo linaendela kufuatilia kwa karibu  maendelo ya watoto kwenye familia ambazo wazazi au walezi walifariki dunia kwa Ebola au wanaoishi kwa kutengwa kwa kuwa karibu na mtu aliyeambukizwa au wanaohitaji msaada wa kisaikolojia ili kukabiliana na hali hiyo.

Halikadhalika inaendelea kufanya kazi kwa karibu na jamii pamoja na serikali ya DRC ili kukomesha janga hilo na pia kutoa msaada wa hali na mali kwa kuzingatia maziko salama kwa marehemu na pia ufuatiliaji katika kampeni ya kuosha mikono na kuunga mkono kuhamasisha wakazi wa mji wa Mbandaka.

Ebola, Mbandaka, UNICEF, Equateur, Gianfranco Rotigliano, DRC