Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukata ni changamoto kwa kazi za G5 Sahel:UN

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akipokelewa na Jenerali Didier Dacko, kamanda mkuu wa vikosi vya G5 Sahel pamoja na vikosi vingine vya Mali alipotembelea makao makuu ya vikosi hivyo mjini Mopti, Mali.
UUN Photo/Marco Dormino
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akipokelewa na Jenerali Didier Dacko, kamanda mkuu wa vikosi vya G5 Sahel pamoja na vikosi vingine vya Mali alipotembelea makao makuu ya vikosi hivyo mjini Mopti, Mali.

Ukata ni changamoto kwa kazi za G5 Sahel:UN

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umetoa wito wa nchi wanachama kushikamana na kusaidia vita dhidi ya mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeida na ISIL kwenye ukanda wa sahel barani Afrika.

Kikosi cha pamoja cha nchi tano za Sahel kutoka Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara kinaendesha operesheni ya pamoja kukabiliana na ugaidi na uhalifu wa kupangwa katika ukanda wa Sahel lakini Umoja wa Mataifa unasema ukata ni changamoto kubwa inayoathiri operesheni hizo na uwezo wa kikosi hicho.

Hayo ni kwa mujibu wa mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa Jean Pierre Lacroix akizungumza leo kwenye kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichokuwa kikijadili kuhusu kikosi hicho cha G5.

Mwaka jana kundi la Sahel linalojumuisha Burkina Faso, Mauritania, Mali, Niger na Chad liliamua kuunda kikosi cha pamoja kupambana na ugaidi. Kikosi hicho kinaweza kwenda popote katika ukanda huo bila matatizo kukabiliana na magaidi wanaovamia na kuwapa hofu kubwa wananchi wa ukanda huo. Wazo la kuunda kikosi cha pamoja chenye uwezo wa kukabili uhalifu  liliungwa mkono na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Makao makuu ya G5 Sahel yaliyoko Mopti Mali, yalishambuliwa na magaidi mnamo tarehe 29 Juni 2018
MINUSMA/Harandane Dicko
Makao makuu ya G5 Sahel yaliyoko Mopti Mali, yalishambuliwa na magaidi mnamo tarehe 29 Juni 2018

Kwa mujibu wa Lacroix ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja sasa asilimia 80 ya wanajeshi wanashiriki katika operesheni hizo . Hata hivyo amesema “Hivi sasa kuliko wakati mwingine wowote wanahitaji msaada wa jumuiya ya kimataifa.”

"Hivi sasa kikosi hicho cha pamoja hakiwezi kutekeleza majukumu yake yote kwa kikamilifu .Wanapungukiwa vifaa , askari, miundombinu ya msingi na hakuna kambi maalumu zilizo salama.”

Lacroix ameushukuru Muungano wa Ulaya kwa juhudi zake kwa kutoa msaada wa kifedha wa kuanzisha kikosi hicho . Ingawa amesema asilimia 50 ya ahadi za fedha zilizotolewa bado haijakusanywa wala kufikishwa zinakohitajika.

Kwa kuongezea amesema bajeti ya mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Mali , MINUSMA ambao unasaidia operesheni za kikosi hicho cha G5 nao una upungufu wa dola milioni 30.

Amesisitiza kwamba mpango huo uko tayari kutoa msaada ulioombwa wa kiufundi na usafiri lakini pia wa kuimarisha kituo cha kijeshi cha vikosi vya Umoja wa Mataifa Mali, lakini kwa ukata uliopo uwezo wake ni mdogo.

Kama alivyosisitiza Lacroix ni vigumu kufikia lengo la usalama Sahel bila kushughulikia mizizi ya mgogoro ikiwemo ukiukwaji wa haki za binadamu na matatizo ya kiuchumi na kijamii.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa watu milioni 24 katika ukanda wa sahel wanahitaji msaada wa kibinadamu , na mbali ya vita na ghasia watu wa ukanda huo wanakabiliwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi na mmomonyoko wa udongo. Lacroix ametoa wito

“Nazitaka nchi zote tano za Sahel kutilia maanani matatizo makubwa kwenye ukanda huo ambayo yanaweka mazingira ya kukaribisha ugaidi.”

Kwa muktadha huu ametoa wito wa mchakato muhimu wa amani nchini Mali akihimiza kwamba ni kitovu cha juhudi za kisiasa za kutatua changamoto za usalama katika ukanda mzima.