Hali katika ukanda wa Sahel inazidi kuwa tete na wananchi ndio waathirika wakubwa-Bintou Keita.

16 Mei 2019

Bintou Keita ambaye ni msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Afrika katika  masuala ya siasa na ujenzi wa amani, hii leo mjini New York ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa hali nchini Mali na neo la Sahel kwa ujumla (Burkina Faso, Mali, Mauritania, Niger and Chad) limesalia kuwa lenye hali ya kutia wasiwasi kuanzia mabadiliko ya tabia nchi yaliyosababisha ukame, kuongezeka kwa kutokuwepo kwa usalama, makundi ya vurugu, usafirishaji haramu wa watu, silaha na madawa.

Bi Keita amenukuliwa akisema, “kama ilivyo ada, wananchi wa kawaida ndio wanaoathirika zaidi na hali hii.”

Kwa mujibu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayofanya kazi katika eneo la Sahel, wakimbizi wa ndani wameongezeka na kufikia zaidi ya 33,000 na wengine 100,000 wamekimbilia katika nchi za jirani.

Aidha Bi Keita ameeleza kuwa vurugu na kukosekana kwa usalama kumeathiri kwa kiasi kikubwa huduma za elimu na afya katika eneo lote la Sahel ambapo zaidi ya shule 1,800 zimefungwa kwa zaidi ya miaka mitatu mfululizo na zaidi ya vituo 80 vimefungwa kabisa au kutoa huduma kwa muda mfupi.

“Haya yote yanatokea wakati makundi ya kigaidi yakiendelea kuongezeka na kutapakaa kote katika mipaka ya ukanda huo ikiwemo ya Burkina Faso, Niger, Benin, Côte d'Ivoire, Ghana na Togo.” Na akaongeza, “wakati hali ya kibinadamu ikizidi kudorora katika Sahel, wakulima wengi wamepoteza msimu mwingine wa kilimo katika eneo la Niger Delta na matokeo yake idadi ya watu wanaotegemea vyakula vya msaada itaongezeka.”

Vile vile Bi Keita amezisihi nchi tano za Sahel kuhakikisha vikosi vinavyoundwa na askari kutoka katika nchi hizo tano kufanya kazi kwa kiwango chao cha juu kurejesha amani katika eneo la Sahel.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter