Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kujiondoa kwa Mali kwenye G5 Sahel na Jeshi la Pamoja ni 'kizuizi' kwa eneo hilo 

Wakazi wa Kaskazini mwa Mali.
© MINUSMA/Gema Cortes
Wakazi wa Kaskazini mwa Mali.

Kujiondoa kwa Mali kwenye G5 Sahel na Jeshi la Pamoja ni 'kizuizi' kwa eneo hilo 

Amani na Usalama

Uamuzi wa nchi ya Mali mnamo Mei 15 kujiondoa katika kundi la G5-Sahel na Jeshi lake la Pamoja ni "bahati mbaya" na "wa kusikitisha", Martha Ama Akyaa Pobee ambaye ni msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Afrika, katika idara  ya masuala ya Siasa, ujenzi wa amani na kulinda amani jana Jumatano ameliambia Baraza la Usalama, huku akizitaka nchi za eneo hilo kuongeza juhudi za kulinda haki za binadamu, huku kukiwa na migogoro ya muda mrefu ya kisiasa na kiusalama. 

Martha Ama Akyaa Pobee, anasema Jeshi la Pamoja liliundwa mnamo 2017 na Wakuu wa Nchi za "G5" ambazo ni Burkina Faso, Chad, Mali, Mauritania na Niger ili kukabiliana na ugaidi katika Sahel. 

Mienendo yenye changamoto 

Hata hivyo, mienendo yenye changamoto ya kisiasa na kiusalama katika Sahel, na matokeo yasiyo na uhakika ya mabadiliko ya Mali na Burkina Faso, tayari yamepunguza kasi ya operesheni za Jeshi la Pamoja la G5 Sahel, wakati huo huo, haijaitisha mkutano wa ngazi ya juu wa kisiasa tangu Novemba 2021, wakati Kamati yake ya Ulinzi na Usalama haijakutana kwa zaidi ya miezi sita. 

Shukrani kwa Kamanda Jenerali Oumar Bikimo, alisema, Jeshi la Pamoja limeweza kufanya operesheni katika sekta zake zote tatu tangu Baraza lilipokutana mara ya mwisho Novemba, licha ya kutokuwepo kwa vikosi vya Mali. 

Jinsi uamuzi wa Mali kuondoka G5 na Jeshi la Pamoja utaathiri mienendo katika kanda ni suala la kusubiri lakini Martha Ama Akyaa Pobee anaona "kwa hakika ni hatua ya kurudi nyuma kwa Sahel," alisema. 

MINUSMA kazini  

Kwa upande wake, ujumbe  wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Mali MINUSMA utaendelea kutoa msaada kwa Wanajeshi wa Pamoja kwa muda wote utakapopewa mamlaka ya kufanya hivyo na Baraza hilo.