Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko G5 huko Sahel kwa kulinda raia-UN

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akisalimu watu baada ya kuzuru msikiti,  Mopti, Mali
UN Photo/Marco Dormino
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akisalimu watu baada ya kuzuru msikiti, Mopti, Mali

Heko G5 huko Sahel kwa kulinda raia-UN

Amani na Usalama

Ukanda wa Sahel unakabiliwa na mashambulizi na shida za mara kwa mara ambapo nchi tano kwenye ukanda huo zimeunda kikosi cha kukabili mashambulizi kiitwacho, G5.

Akiwa Mopti, jimbo lililoko katikati mwa Mali, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametembelea kambi ya askari wa kundi la nchi 5 za ulinzi wa ukanda wa Sahel, G5 du Sahel iliyoko eneo la Sevare, na kupongeza wanawake na wanaume wanaounda kikosi hicho na ambao wamejitolea kulinda raia kwenye eneo hilo.

Amesema kundi hilo pamoja na kutoa hakikisho la usalama kwa raia, pia ni hakikisho kwa jamii ya kimataifa dhidi ya ugaidi na uhalifu wa kupangwa.

Kikosi hicho cha G5 du Sahel kinaundwa na nchi tano ambazo ni Burkina Faso, Chad, Mali, Mauritania na Niger.

Bwana Guterres amesema angalipenda kuona kundi hilo linapatiwa usaidizi zaidi akisema kuwa..

“Tumependekeza mfumo wa ufadhili wenye hakikisho ambao utawezesha kikosi hiki kupanga mipango yake ya baadaye bila ugumu wowote.”

Kikosi hicho kiliundwa mwezi Februari mwaka 2014 ambapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nalo mwaka 2017 lilipitisha azimio la kuridhia usaidizi wa kiufundi kwa kikosi hicho.

“Tunapaswa kuisihi zaidi jamii ya kimataifa ili iweze kuchangia rasilimali za kifedha na vifaa ambazo ni muhimu. Halikadhalika tunaiomba jamii ya kimataifa iwekeze katika maendeleo ya ukanda huo wa Sahel kwa kuwa hakuna amani  bila usalama, na hakuna maendeleo bila amani.”

 

António Guterres atembelea msikiti Mopti, Mali.
UN Photo/Marco Dormino
António Guterres atembelea msikiti Mopti, Mali.

Akiwa Mopti, Katibu Mkuu alitembelea msikiti mmoja na kuwa na mazungumzo na imam wa msikiti huo.

Halikadhalika tayari amefika kwenye makao makuu ya kikanda ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kusimamia utulivu nchini Mali, MINUSMA ambako anakutana na viongozi wa kidini na kijamii.

Mapema jana,  Bwana Guterres alishiriki maadhimisho ya miaka 70 ya ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa mjini Bamako na kusisitiza kutambua mchango wa walinda amani wanaojitolea kutwa kucha kulinda raia kwenye maeneo hatarishi zaidi duniani.