Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakulima na wafugaji wana ufunguo wa kuepusha usugu wa dawa- FAO

Mwanamke akishughulikia kuku aliowafuga San Nicolas, Colombia.
World Bank/Charlotte Kesl
Mwanamke akishughulikia kuku aliowafuga San Nicolas, Colombia.

Wakulima na wafugaji wana ufunguo wa kuepusha usugu wa dawa- FAO

Afya

Maadhimisho ya wiki ya  kuhamasisha umma kuhusu matumizi ya viuavijasumu ikiendelea, Umoja wa Mataifa umesema wakulima wana dhima muhimu katika kupunguza usugu wa dawa hizo kwa kutumia mbinu bora za usafi katika shughuli zao za kila siku.

Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO limesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuzingatia kuwa viuavijasumu hutumika pia kwa mifugo ya Wanyama, ufugaji wa samaki na hata hunyunyuziwa kwenye mazao na matunda ili kudhibiti magonjwa ya wanyama na mazao ya chakula.

Afisa mkuu wa mifugo FAO Juan Lubroth amesema iwapo dawa za kuua vijiumbe maradhi zitatumiwa kwa kupita kiasi mashambani, wakulima watakuwa wanachangia katika kuenea kwa usugu wa dawa hizo na hivyo vijidudu kuhamia kwenye mazingira kupitia vinyesi vya wanyama na mazao.

“Zinaweza kuchafua mifumo yetu ya chakula na mnyonyoro mzima wa usambazaji wa mazao sokoni, ikimaanisha kutoka mashambani na mazizini hadi mezani,” amesema Bawna Lubroth.

Hivyo ametaja baadhi ya hatua ambazo wakulima na wafugaji wanaweza kutumia ili kuwa walinzi wakuu dhidi ya kuenea kwa usugu wa dawa za kuua vijiumbe maradhi.

Hatua hizo ni pamoja na  Wakulima wahakikishe mara kwa mara wanafanya usafi kwenye vioski vyao vya kuhifadih dawa, mabwawa ya samaki na vifaa vya kilimo kama njia mojawapo ya kuondokana na vijidudu ambavyo vinaweza kusababisha magonjwa kwa wanyama.

Halikadhalika wasafishe mavazi yanayotumika mashambani na mazizini ikiwemo viatu na bila kusahau kusafisha mikono punde tu baada ya kuhudumia shamba au mifugo.

Bwana Lubroth ametaja hatua nyingine ni kuhakikisha mifugo ya aina moja na yenye umri mmoja inawekwa pamoja baada ya kuchanganya aina tofauti sambambana kusafisha mabanda au mazizi pindi mifugo inapouzwa.

Hatua nyingine ni kuhakikisha mifugo inayougua inatengwa na mingine.

“Hizi ni hatua rahisi ingawa bado inahitajika uwekezaji mkubwa ili kudhibiti usugu wa viuavijasumu kwa kutambau kuwa kilimo safi kinaleta pia mapato mengi” amesema afisa huyo wa FAO.

FAO imesema kuwa ni vyema kuhakikisha kuwa usugu wa viuavijasumu unadhibitiwa kwa kuwa ni tishio kubwa kwa binadamu ambapo katika kila dakika moja, mtu mmoja anafariki dunia kutokana na maambukizi yatokanayo na usugu wa dawa.

“Bila kuchukua hatua, idadi hiyo itaongezeka na ifikapo mwaka 2050, tishio la usugu wa dawa za kuua vijiumbemaradhi utagharimu dola trilioni 6 kila mwaka,” imesema FAO.