Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Acheni kutumia viuavijasumu kukuza mifugo-FAO

FAO yaanzisha Kampeni ya chanjo ya mifugo magharibi mwa Aweil nchini Kusini ikifadhiliwa na Benki ya Dunia. Picha: FAO

Acheni kutumia viuavijasumu kukuza mifugo-FAO

Afya

Umoja wa Mataifa umetaka wafugaji kuacha mara moja tabia ya kutumia viuavijasumu kukuza mifugo yao pamoja na kuku, ukisema kuwa dawa hizo ni kwa ajili ya matibabu na si vinginevyo.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, Jose Graziano da Silva amesema hayo huko Roma, Italia wakati huu ambapo inaelezwa kuwa wafugaji wa wanyama na kuku wanatumia dawa hizo ili kuharakisha ukuaji wa mifugo yao.

"FAO inachechemua matumizi ya viuavijasumu kwa ajili ya matibabu ya magonjwa na kupunguza machungu mengine ya wanyama na dawa hizo zinapaswa zitumike katika mazingira yenye udhibiti ili kuzuia maambukizi ya magonjwa,” amesema da Silva.

Amesema ongezeko la matumizi ya viuavijasumu kwa binadamu na wanyama katika mazingira yasiyo sahihi, limesababisha usugu wa madawa hayo, jambo linaloweza kuleta hasara ya dola zaidi ya dola trilioni milioni 100 kwa mwaka.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa FAO amesema ingawa nchi 89 pekee zimesema zimeweka mfumo wa kukusanya takwimu za matumizi ya viuavijasumu kwa wanyama, bado hiyo haitoshelezi, lazima hatua zichukuliwe zaidi.

Amezitaka serikali na mashirika ya kiraia kuimarisha ushirikiano wao ili kusaidia kuondokana na matumizi hayo kwa lengo la kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.