Tuzingatie matumizi sahihi ya dawa kuiokoa dunia na usugu wa dawa-FAO

12 Novemba 2018

Juma hili ni wiki ya kuelimisha umma kuhusu matumizi ya viuavijasumu ambavyo inaelezwa kuwa matumizi yasiyo sahihi yanasababisha usugu dhidi ya vijiumbe maradhi. 

Kampeni hiyo inapigiwa chepuo na mashirika ya Umoja wa Mataifa  ikiwemo lile la afya, WHO na lile la chakula na kilimo, FAO ambapo mtaalam wa mawasiliano wa FAO Christine Czeniak  anaamini kuwa wakulima wana mchango mkubwa katika kuzuia kuenea kwa usugu wa dawa za kuua vijiumbe maradhi.

Kwanza Christine anaeleza kuwa usugu wa dawa ni pale ambapo vijidudu vinavyosababisha maradhi, vinapotengeneza uwezo wa kushindana na dawa na akifafanua kuhusu ukubwa wa tatizo linalosababishwa na usugu wa dawa anasema,

Hili ni tatizo la dunia nzima ndiyo maana tunatakiwa kujali na kuchukua hatua. Kwa kutizama kidunia, kwa sasa kila dakika mtu mmoja anafariki dunia kutokana na usugu wa vijidudu dhidi ya dawa na idadi hii itazidi kupanda”

Na kuhusu ni eneo gani la dunia ambalo limeathirika zaidi Bi. Czeniak anasema kwa bahati mbaya maeneo yenye kipato kidogo yameathirika zaidi na kwa hivyo yatabeba mzigo mkubwa zaidi.

Na kuhusu nini kifanyike ili kupambana hali hii ya usugu wa dawa? Bi. Czeniak  anasema dunia haiwezi kuacha kutumia viuavijasumu au viuavijiumbe maradhi kwani kuna maradhi ambayo yako kwenye wanyama na yasipodhibitiwa yanaweza kuwaathiri wanyama na wanadamu lakini muhimu ni kutumia dawa hizi kwa usahihi na pindi tu zinapohitajika.

Lakini FAO inafanya nini kuwasaidia wakulima? Bi. Czeniak  anasema,

“Unaweza kuwa na kanuni na kuwaambia watu namna ya kutumia viuavijasumu lakini mwisho wa siku ni watu wenyewe kuamua jinsi ya kutumia tofauti. Kwa hivyo kuna mradi ambao umedhaminiwa na Uingereza ambao FAO inafanya katiika nchi 12 barani Afrika na Asia kuongea na wakulima na wauza dawa za mifugo ili kubadili tabia ya namna wanavyotumia dawa”

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud