Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dawa za kuua vijiumbe maradhi bado zinauzwa kiholela- Ripoti

Usugu wa dawa za kuua vijiumbe unazuia uzuiaji na matibabu ya maambukizi yanayosababishwa na ikiwemo viini.
Picha: WHO
Usugu wa dawa za kuua vijiumbe unazuia uzuiaji na matibabu ya maambukizi yanayosababishwa na ikiwemo viini.

Dawa za kuua vijiumbe maradhi bado zinauzwa kiholela- Ripoti

Afya

Ripoti mpya iliyotolewa na mashirika ya Umoja wa Mataifa hii leo imesema licha ya hatua za kudhibiti usugu wa dawa dhidi ya vijiumbe maradhi, AMR, bado kuna changamoto kubwa katika utekelezaji wa makubaliano na hivyo hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa.

Mashirika hayo lile la afya duniani, WHO, la chakula na kilimo FAO na lile la afya ya Wanyama OIE yamesema tathmini katika mataifa 154  yameonyesha pengo katika hatua za kudhibiti usugu huo miongoni mwa nchi hizo.

Mathalani ripoti inasema nchi za Ulaya zimekuwa na sera za kudhibiti usugu wa dawa za kuu vijiumbe maradhi kwa binadamu na wanyama kwa miongo zaidi ya minne, ilhali nchi nyingine hususan za kipato cha chini bado kasi ni ndogo.

Changamoto kwenye nchi hizo za kipato cha chini ni ufuatiliaji, elimu na kuweka udhibiti wa matumizi ya dawa hizo za kuuwa vijiumbe maradhi kama ilivyotangazwa kwenye mpango wa kimataifa wa utekelezaji wa mwaka 2015.

“Dawa za kuua vijiumbe maradhi zinapatikana kiholela mitaani na hakuna ukomo wa matumizi yake,” imesema ripoti hiyo ikiongoza kuwa baadhi ya dawa ambazo zinapaswa kuuzwa tu baada ya mteja kuwasilisha cheti cha daktari, bado zinauzwa bila kufuata masharti hayo.

Ripoti imesema kitendo hicho kinaweka hatarini afya za binadamu na wanyama na hivyo kusababisha usugu wa dawa hizo za kuua vijiumbe maradhi.

Kwa upande mwingine ripoti imegusia hatua zilizochukuliwa na mataifa 67 ya kutunga sheria za kudhibiti uzalishaji na usambazaji wa dawa hizo kwa ajili ya matumizi kwa wanyama.

Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi msaidizi wa WHO anayehusika na usugu wa viua vijiumbe maradhi, Dkt. Ranieri Guerra amesema ni dhahiri kuwa sasa kuna mwelekeo wa kudhibiti usugu wa dawa 

hizo.

Hata hivyo ametoa wito kwa serikali kuazimia kudhitbiti matumizi holela ya dawa hizo katika sekta zote za afya ya binadamu, wanyama na mimea, akisema kuwa kinyume na hivyo kuna hatari ya kupoteza fursa ya matumizi ya dawa hizo adhimu.

Kwa upande wake, Maria Helena Semedo ambaye ni Naibu Mkurugenzi wa FAO amekaribisha suala kwamba nchi zinachukua hatua kutumia vyema dawa hizo kwenye kilimo lakini ametaka udhibiti wa zaidi wa matumizi holela.

Takwimu zinaonyesha kuwa mataifa 100 hivi sasa yana mipango ya kitaifa  kuhusu matumizi ya dawa hizo za viua vijiumbe maradhi ilhali 51 ziko kwenye mwelekeo wa kuandaa mipango hiyo.