Jimbo la Anbar lasaka mbinu za matumizi bora ya vifusi vya majengo yaliyobomolewa

12 Novemba 2018

Nchini Iraq kwenye jimbo la Anbar, kumefanyika warsha yenye lengo la kuangalia jinsi ya kuanzisha vituo vya kurejeleza taka za vifusi vilivyolundikana kwenye eneo hilo baada ya mapigano yaliyowezesha kufurushwa kwa magaidi wa ISIL.

Makala ya shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP inasema vifusi hivyo ambavyo vimetapakaa na kutishia siyo tu usalama wa afya ya binadamu bali pia uchafuzi wa mazingira vinaweza kutumika katika jitihada za ujenzi mpya wa nchi hiyo.

Naibu Gavana wa Anbar Mustapha Arsan amesema “kwa zaidi ya miaka miwili tangu kutwaa maeneo mengi kutoka kwa ISIL mwaka 2016, vifusi vimeendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa makumi ya maelfu ya wakimbizi wa ndani kurejea kwenye makazi yao, kuanza upya maisha yao na hata kuanzisha biashara.

Wawakilishi wa manispaa za miji iliyoharibiwa zaidi ya Ramadi, Haditha, Hit, Qaim na Kubaisa, nao walielezea matatizo makubwa ya kuendelea kuondoa kiwango kikubwa cha vifusi hivyo , wakitaja ukosefu wa vifaa na fedha za kutekeleza mpango huo.

 

Msichana akichungulia akiwa ndani ya nyumba iliyoharibiwa katika mapigano ya Ramadi, Anbar, Iraq.
Photo: UNICEF/Wathiq Khuzaie
Msichana akichungulia akiwa ndani ya nyumba iliyoharibiwa katika mapigano ya Ramadi, Anbar, Iraq.

Akizungumza kwenye warsha hiyo, Salah Thameel, mhandisi kutoka Chuo Kikuu cha Anbar amesema utafiti wake umebaini kuwa taka za vifusi kutoka Ramadi ambazo zimepondwapondwa zina ubora wa hali ya juu na zinakidhi viwango vya Iraq vya kuweza kutumika kwenye ujenzi wa barabara.

Amesema gharama za kuponda vifusi hivyo kuwa kokoto ni theluthi moja ya gharama ya kununua kokoto zenyewe na hivyo hata ukiweka gharama za usafirishaji bado gharama  yake inakuwa ni nafuu.

Bwana Thameel ameongeza kuwa, “kwa kutumia tena vifusi hivyo vilivyopondwa, tunakuwa tumepunguza madhara ya kimazingira ya kwenya mashimo ya  kokoto na pia uchafuzi wa hewa utokanao na vumbi la kwenye mashimo hayo.

 

Raia wa Iraq wasio na makazi kutoka wilaya ya Ramadi katika mkoa wa Anbar.
Photo: UN Iraq
Raia wa Iraq wasio na makazi kutoka wilaya ya Ramadi katika mkoa wa Anbar.

Akiunga mkono hoja hiyo, Rais wa kamati ya afya na mazingira na mjumbe wa baraza la jimbo, Asmaa Osama amesema “kupondaponda upya vifusi hiyo na kutumia, sit u kutarahisha uondoaji wa malundo ya vifusi vya majengo bali pia kutapunguza gharama.”

Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 80 ya wakazi wa Ramadi, mji mkuu wa jimbo la Anbar, lenye watu wapatao 570,000, wanaishi kwenye magofu.

Hadi sasa tani milioni tatu za vifusi vya majengo yaliyobomolewa huko Anbar, kati ya tani milioni saba zimeshaondolewa kwa msaada wa shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP.

Hata  hivyo kiwango kilichosalia kimechanganyika na vilipuzi ambavyo bado  havijalipuka.

Warsha hiyo iliyoandaliwa kwa ushirika kati ya wizara ya afya ya Iraq na UNEP imefanyika jimbo la Anbar na kuleta pamoja wadau mbalimbali wakiwemo wataalamu wa kiufundi, wasomi, wataalamu wa kutegua mabomu na mashirika ya Umoja wa Mataifa.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter