Mizozo inapopamba moto, mazingira nayo huwa hatarini- UNEP

Kituo cha maji cha Abu Shouk katika kambi ya wakimbizi wa ndani, Darfur, Sudan ambako vita vinaathiri mazingira.
UNAMID/Albert González Farran
Kituo cha maji cha Abu Shouk katika kambi ya wakimbizi wa ndani, Darfur, Sudan ambako vita vinaathiri mazingira.

Mizozo inapopamba moto, mazingira nayo huwa hatarini- UNEP

Tabianchi na mazingira

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kuzuia uharibifu wa mazingira kwenye maeneo ya mizozo na vita, Umoja wa Mataifa umeweka bayana sababu za kulinda mazingira ikitolea mfano maeneo sita ambako bayonuai imeharibiwa kutokana na vita. 

Shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP limesema maeneo hayo ambayo ni theluthi mbili ya maeneo yenye bayonuai muhimu duniani yamekumwa na mizozo na hivyo kutishia harakati za uhifadhi wa mazingira.

Miongoni mwao ni huko Vietnam ambako kemikali Agent Orange iliyotumiwa na Marekani wakati wa vita vya Vietnam kwa takribani muongo mmoja kuanzia mwaka 1961 hadi 1971, wakati wa vita vya Vietnam ili haribu mazingira.

“Jeshi la Marekani lilipuliza mamilioni ya lita za kemikali hiyo kwa lengo la kukausha uoto wa majani maeneo ya kusini mwa Vietnam,” imesema taarifa ya UNEP ikiongeza kuwa lengo lilikuwa kuharibu msitu na kufukuza wapiganaji wa msituni wa kundi la Viet Cong na sasa misitu hiyo imeharibiwa.

Eneo lingine ni Afrika hususan nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambako tangu katikati ya miaka ya 1990, mapigano  yamekuwa na madhara makubwa kwa wanyama wa msituni ambao ni kitoweo cha nyamapori kwa wapiganaji, raia na wafanyabiashara.

UNEP inasema mzozo wa DRC pia unahusisha udhibiti wa maliasili kama vile madini na mbao ambavyo ni vyanzo vya mapato kwa pande husika.

“Mzozo wa DRC na matokeo yake ya kutokuwepo kwa sheria, vimekuwa chimbuko la vitendo kama vile ukataji misitu holela sambamba na michakato hatarishi ya uchimbaji majini,” imesema UNEP.

Maeneo mengine ni Colombia, Nepal, Afghanistan na Iraq.

Shirika hilo limesema kuwa zama za vita zinaweza kuongeza kasi ya  uharibifu wa  mazingira kwa kuwa watu wanahaha kusongesha maisha yao huku mifumo ya usimamizi wa mazingira ikiwa imesambaratishwa na hivyo baiyonuai kuharibika.

Maadhimisho ya mwaka ya siku ya kuzuia uharibifu wa mazingira kwenye mizozo ni  ya 17 na yaliidhinishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2001.