Mkimbizi kutoka DRC achagiza kuokoa wakimbizi watokanao na mabadiliko ya tabianchi

7 Januari 2019

Kijana mmoja mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambaye sasa anaishi nchini Marekani amechukua hatua ya  uchechemuzi ili kuhakikisha siyo tu wakimbizi watokanao na mabadiliko ya tabianchi wanapatiwa msaada bali pia vijana wanashika hatamu katika kulinda na kuhifadhi mazingira.

Kijana huyo Kibiriti Majuto mwenye umri wa miaka 20 amesema hayo akihojiwa na shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP wakati huu ambapo kipaumbele zaidi kimekuwa kikielekezwa kwa wakimbizi watokanao na mizozo, majanga na usafirishaji haramu.

Kwa mujibu wa utafiti uliofadhiliwa na Chuo Kikuu cha Oxford na shirika la kuhudumia wakimbizi duniani, UNHCR pamoja na serikali za Norway na Uswisi, kati ya watu milioni 50 na 200 wanatarajiwa kuwa wakimbizi watokanao na mabadiliko ya tabianchi ifikapo mwaka 2050.

Katika kutekeleza azma yake, kijana Kibiriti ameanzisha jukwaa liitwako Zero Hour ambalo linachochea serikali kuangalia upya neno la wakimbizi watokanao na mazingira ili kuziba pengo la haki zao za ulinzi na uhifadhi.

OCHA/UNDAC
Mama na mwanae wakijaribu kujiokoa kwenye mafuriko yaliyokumba jimbo la Niger nchini Nigeria. Mafuriko yanatokana na mvua zinazonyesha jimboni humo tangu katikati ya mwezi Julai mwaka huu.

“Hii ni hatua muhimu ya kwanza ili kusaidia sera kwa wale ambao wamelazimika kukimbia kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Tumesihi serikali za nchi tajiri kukaribisha kwenye nchi zao wakimbizi hawa kwa kuwapatia maeneo salama,” amesema Kibiriki akiongeza kuwa “jumuiko letu bado change na mimi kama mkimbizi ningalipenda kuona linafanya kazi zaidi kwa wakimbizi. Hivi sasa sioni kama uhamiaji ni fursa ya mtu anachagua.”

Alipoulizwa kuhusu nafasi ya vijana kwa kuzingatia kuwa katika maandamano ya mwezi Julai mwaka 2018 waandamanaji walipaza sauti wakisema “vijana kwa hatua za mabadiliko ya tabianchi hivi sasa,” Kibiriti amesema hilo halina ubishi.

Amesema “harakati dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira ni vita kwa ajili ya mustakabali wetu. Hii ndio maana tunataka vijana wasimame kidete kuchukua hatua kwenye miji yao, serikali na nchi zao.”

Kibiriri amesema kuna mambo mengi vijana wanaweza kufanya “kama vile kupigia kura wagombea ambao ni watetezi wa tabianchi, kupunguza ulaji wa  nyama, kupunguza matumizi ya nishati isiyo endelevu na hata kufundisha stadi bora za kupika zisizoharibu mazingira.”

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud