Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika yapitisha mpango wa miaka 10 wa afya na mazingira:UNEP

Mtoto Kadia alizaliwa akiwa ameambukizwa ugonjwa ambao ni hatari kwa watoto wachanga. Hata hivyo nafuu yake ni kwamba aliweza kupata dawa ya viuavijasumu punde tu baada ya kuzaliwa la sivyo angalifariki dunia. Pichani akipatiwa dawa na muuguzi nchini Mali
© UNICEF/UN0188875/Njiokiktjien
Mtoto Kadia alizaliwa akiwa ameambukizwa ugonjwa ambao ni hatari kwa watoto wachanga. Hata hivyo nafuu yake ni kwamba aliweza kupata dawa ya viuavijasumu punde tu baada ya kuzaliwa la sivyo angalifariki dunia. Pichani akipatiwa dawa na muuguzi nchini Mali

Afrika yapitisha mpango wa miaka 10 wa afya na mazingira:UNEP

Afya

Mawaziri wa afya na mazingira kutoka barani Afrika leo wamekubaliana kuwa na mpango wa miaka 10 wa kuongeza uwekezaji na kusongesha mbele vipaumbele vya afya na mazingira.

Mkakati huo wa 2019-2029 wa Muungano wa Afrika umepitishwa wakati wa kufunga mkutano wa tatu wa mawaziri wa afya na mazingira uliofanyika nchini Gabon kuanzia Novemba 6 hadi 9.

Mawaziri hao wamekubaliana kuimarisha mifumo ya sera na taasisi kwa ajili ya kuchukua hatua na kuanzisha mbunu bunifu za kupata ufadhili , ikiwemo kujumuisha rasilimali za ndani zaidi zilizotengwa kwa ajili ya hatua za pamoja za afya na mazingira.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira UNEP mkakati huo utakuwa ditra ya kuhakikisha malengo ya maendeleo endelevu yaani SDGs yahusuyo mazingira yanapatiwa kipaumbele kinachostahili.

Katika ujumbe wake kwa njia ya video kwenye mkutano humo mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani Dkt. Tedros Adhamo Ghebreyesus amesema “Muungano wa afya na mazingira barani Afrika unawakilisha mfano imara wa ushirikiano kitu ambacho tunakihitaji ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu.”

Naye waziri mkuu wa Gabon Franck Emmanuel Issoze-Ngondet mwenyeji wa mkutano huo amesema “Ni lazima tuende mbali zaidi husuani katika kukusanya rasilimali na fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mipango ya kitaifa lakini pia katika kufafanua na kushirikiana majukumu.”

WHO inasema karibu kifo kimoja kati ya vine vya mapema barani Afrika vinahusiana na mazingira na mabadiliko ya tabia nchi na vinatishia kuongeza idadi ya dharura za kiafya na milipuko katika miaka ijayo.

Viongozi wa Afrika wametambua haja ya sekta za afya na mazingira kufanyakazi pamoja tangu azimio la Librevile la mwaka 2008 na azimio la Luanda la mwaka 2010 kupelekea kuanzishwa kwa muungano wa kimkakati wa afya na mazingira ambao unaonekana kama dira.

Naye mkuu wa UNEP Erik Solheim akizungumfa wakati wa kufunga mkutano huo amesema ukuaji wa haraka na usio wa mpangilio wa miji barani na viwanda Afrika unaongeza hatari ya magonjwa sugu kama saratani, maradhi ya moyo na kiarusihivyo ametsisitiza “ Ni lazima tuchukue hatua dhidi ya uchafuzi wa hewa na mazingira , ambavyo ni chanzo kikubwa cha vifo vya binadamu kwani hukatiki maisha ya watu milioni 7 kila mwaka . Serikali, makampuni ya biashara na raia wanachukua hatua za kupambana na uchafuzi wa hewa na uharibifu wa mazingira , lakini hazitoshi tunahitaji kufanya zaidi ya hayo.”

Mawaziri wamemtaka mwenyeji wa mkutano huo kuwasilisha mpango huo kwa ajili ya kupitishwa na Muungano wa Afrika na matokeo kusaidia katika Baraza kuu la nne na mazingira litakalofanyika Nairobi Kenya kuanzia Machi 11-15 mwaka 2019.