Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matatu zasababisha uchafuzi wa hewa Nairobi, Kenya-UNEP

Matatu mjini Nairobi Kenya
UN Environment/Jack Kavanagh
Matatu mjini Nairobi Kenya

Matatu zasababisha uchafuzi wa hewa Nairobi, Kenya-UNEP

Afya

Kitendo cha baadhi ya magari ya kusafirishia abiria maarufu kama MATATU kwenye mji mkuu wa Kenya, Nairobi, kuacha injini zao zinawaka muda mrefu wakisubiri abiria, kimeripotiwa na shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP, kusababisha uchafuzi wa mazingira. 

“Wa mwisho, tunaondoka , tunaondoka, wa mwisho kwenda Athi River,” 

Hivyo ndivyo anapaza sauti dereva wa Matatu Samuel Mburu akiwaita abiria ili wapande basi hilo mjini mjini Nairobi, lakini nusu saa baadaye Mburu akiwa ndani ya matatu yake iliyochorwa rangi za kuvutia bado yupo kwenye kituo cha basi akisubiri abiria.

Yeye anasema sababu ya kuacha injini ya matatu ikiwaka ni kwa ajili ya kuvutia wateja ili waamini kuwa wanaondoka muda si mrefu, lakini katika dakika hizo thelathini hewa chafuzi imetolewa na gari lake.

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limesema chembechembe ndogo sana za vyuma, vumbi na kemikali kutoka kwenye moshi utolewao na injini vyuma au vumbi vinaweza kupenya kwenye mapafu na kusababisha magonjwa ya moyo na mapafu.

WHO inakadiria kuwa watu takriban 19,000 hufariki dunia kila mwaka nchini Kenya kutokana na hewa chafuzi ambapo shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP inataja viwango vya uchafuzi vikiwa asilimia 70 juu ya viwango salama mjini Nairobi.

Mabasi  hayo ya abiria yametajwa kuwa hatari kwani hupatikana pia karibu na shule na kuweka hatarini watoto ambao wako katika hatari zaidi ya madhara yatokanayo na hewa chafuzi kwa sababu watoto wanapumua haraka kuliko watu wazima na hivyo kuvuta hewa chafuzi zaidi wakati ambapo miili yao na ubongo unakomaa.

“Nina shida ya kupumua, wakati mwingine ninakohoa vumbi nyeusi kwa sababu natumia muda mwingi karibu na matatu,”

Mmoja wa wamiliki wa kampuni za mabasi mjini Nairobi, Dennis Ngunugu amenukuliwa akisema “nina shida ya kupumua, wakati mwingine ninakohoa vumbi jeusi kwa sababu natumia muda mwingi karibu na matatu,”

Hali ni kama hii kwa abiria na madereva wa matatu ambapo UNEP imesema kunahitajika kuwa na maabadiliko ya kitamadunia ambapo madereva wanazima injini za gari na hiyo itasaidi kupunguza uchafuzi.

Aidha UNEP imeongeza kuwa kunapaswa kuwa na tofauti katika mipango miji ili kuondokana na mipango inayotegemea usafiri wa magari na kupanga miji kuwawezesha watu kutembea au kuendesha baiskeli.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.