Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya kibinadamu Batangafo, CAR si shwari

Maafisa polisi kutoka ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini  Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR wakiwa kwenye doria mjini Bouar nchini humo  katika picha hii ya Agosti 2018
MINUSCA/Hervé Serefio
Maafisa polisi kutoka ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR wakiwa kwenye doria mjini Bouar nchini humo katika picha hii ya Agosti 2018

Hali ya kibinadamu Batangafo, CAR si shwari

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, umelaani janga la kibinadamu linaloendelea kwenye eneo la Batangafo mkoani Ouham kaskazini-maghaibi mwa nchi hiyo.

Naibu Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MINUSCA Najat Rochdi ametoa kauli hiyo ya kulaani alipozungumza na waandishi wa habari kwenye mji mkuu wa CAR, Bangui baada ya kuzuru eneo hilo tarehe 4 mwezi huu ambako alishuhudia hali duni za kibinadamu za wakimbizi wa ndani 30,000 waliopoteza kila kitu chao kutokana na ghasia zilizoibuka kwenye eneo hilo tarehe 31 mwezi uliopita.

Mapigano hayo kati ya kikundi cha anti-Balaka na waliokuwa wafuasi wa Seleka yaliibuka  baada ya mkinzano ndani ya makundi hayo, hali iliyoambatana na uporaji wa mali za raia.

Baada ya kushuhudia hali halisi akiwa na wawakilishi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo la kuhudumia watoto, UNICEF, mpango wa chakula, WFP, afya WHO, wakimbizi, UNHCR na misaada ya kibinadamu OCHA, Bi. Rochdi amesema “kiwango hiki cha kukata tamaa hakikubaliki. Nimeshuhudia hali ya udharura iliyochochewa na mashambulio hayo. Moto uliteketeza zaidi ya mahema 5,100 pamoja na soko na kusababisha watu wapatao 30,000 kukimbia makazi yao.”

Bi. Rochdi ambaye pia ni mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa huko CAR amesisitiza kuwa licha ya  uwepo wa kiwango kikubwa cha mahitaji ya kibinadamu, tayari wameanza kugawa misaada muhimu kama vile dawa na chakula.

Ameshukuru watoa huduma za kibinadamu ambao wameendelea kusalia Batangafo licha ya shinikizo la ukosefu wa usalama akisema “katu hatutokata tamaa.”

Kuhusu udhibiti wa hali ya usalama, Naibu Mkuu huyo wa MINUSCA amesema tayari ujumbe huo wa kuweka utulivu CAR umepeleka kikosi mahsusi cha kuhakikisha usalama wa raia huku akihoji utiifu wa wafuasi wa zamani wa anti-Balaka na Seleka ambao walichochea mzozo wa mwisho wa mwezi uliopita licha ya kutia saini makubaliano ya amani kwenye eneo lao.

“Lazima wawajibishwe. Hawawezi kusema kuwa wanashiriki kwenye mazungumzo na mchakato wa amani na wakati huo huo wanaumiza raia,” amesema Bi. Rochdi.

Pamoja na kuongeza walinda amani huko Batangafo, MINUSCA imesema inaendelea na doria huko Bambari, licha ya shambulio dhidi ya ujumbe huo na lililofanywa na kikundi cha UPC ambacho kimemeguka kutoka Seleka.

MINUSCA imekumbusha kuwa katika operesheni zake huko Bambari katu hailengi raia wala jamii yoyote licha ya ulaghai kutoka wafuasi hao wa zamani wa Seleka.