Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake, wanaume, wasichana na wavulana CAR wamepoteza matumaini- OCHA

Mwanamke akiwa Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati
UN Photo/Eskinder Debebe)
Mwanamke akiwa Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati

Wanawake, wanaume, wasichana na wavulana CAR wamepoteza matumaini- OCHA

Amani na Usalama

Janga la kibinadamu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR linazidi kupamba moto likichochewa na ongezeko la watu wanaolazimika kukimbia makwao, ukosefu wa usalama na vikwazo wanavyokabiliana navyo wafanyakazi wa kibinadamu.

Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mjini Geneva, Uswisi na Bangui, na ofisi ya Umoja wa Mataifaya kuratibu misaada ya  kibinadam, OCHA ikimnukuu mratibu wa masuala ya kibinadamu wa umoja huo nchini CAR, Najat Rochdi.

Bi. Rochdi amesema katika wiki tatu zilizopita, zaidi ya watu 50,000 wamekumbwa na zahma huko Batangafo mkoani Ouham na Alindao mkoani Basse Kotto ambako vituo viwili vya kuhifadhi wakimbizi wa ndani vilitiwa moto.

“Dunia haiwezi kufumbia macho kile kinachoendelea, CAR. Tumerejea katika hali ya zamani ya mzozo,. Mashambulio haya yanagharimu maisha ya wanawake, wanaume, wasichana na wavulana wasio na hatia. Wamepoteza kila kitu ikiwemo matumaini,” amesema Bi. Rochdi akiongeza kuwa  ingawa watoa huduma za misaada wanaendelea kugawa misaada kwenye maeneo mengine, katika miji ya Batangafo na Alindao lazima kazi ianze upya kabisa.

Bi. Rochdi amelaani vikali ongezeko la mashambulio dhidi ya raia na miundombinu na ametoa wito kwa pande zote husika kwenye mzozo huko CAR zizingatie sheria za kimataifa za haki za binadamu na kibinadamu.

“Raia hususan wanawake na watoto wanaendelea kubeba mzigo wa mzozo huu na wako hatarini zaidi kupata matatizo kutokana na ukosefu wa ulinzi,” amesema mratibu huo wa Umoja wa Mataifa.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa takribani watu milioni 2.9 wanahitaji msaada na ulinzi nchini CAR wakati huu ambapokila mwezi kuna matukio yapatayo 1000 yahusianayo na  ukosefu wa usalama.

Licha ya mashambulizi dhidi ya raia, watoa huduma za misaada nao wanalengwa ambapo mwezi Oktoba pekee kulikuwepo na matukio 338 ya mashambulizi dhidi ya wafanyakazi hao kwenye taifa hilo ambalo ni hatari zaidi duniani kwa watoa misaada.

Mahitaji ya kibinadamu nchini CAR yakizidi kuongezeka, Umoja wa Mataifa unasema bado kuna pengo kubwa la ombi la usaidizi kwa mwaka huu ambapo hadi sasa wamepokea dola milioni 240 tu kati ya dola milioni 515 zilizoombwa.

Kwa mantiki hiyo, “fedha zaidi zinatakiwa ili kuweka kukidhi mahitaji muhimu na ya kidharura ambayo yanaibuka nchini humo,” amesema Bi, Rochdi.