Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfumo wa kudhibiti Polio Nigeria kutumika kufanikisha afya kwa wote- WHO

Mama na mwana wapewa chanjo dhidi ya magonjwa ya kuambukizwa. Chanjo nyingi hutokea baada ya milipuko ya magonjwa  kama vile Polio, Kipindupindu na magonjwa mengine.
UNICEF/ Nangyo
Mama na mwana wapewa chanjo dhidi ya magonjwa ya kuambukizwa. Chanjo nyingi hutokea baada ya milipuko ya magonjwa kama vile Polio, Kipindupindu na magonjwa mengine.

Mfumo wa kudhibiti Polio Nigeria kutumika kufanikisha afya kwa wote- WHO

Afya

Shirika la afya duniani WHO linajadiliana na serikali ya Nigeria kuona jinsi gani wanaweza kutumia mfumo wa kukabiliana na polio ili kufanikisha huduma ya afya kwa wote nchini humo.

Hatua hiyo ya WHO inazingatia mafanikio ya mfumo huo uliowezesha kudhibiti ugonjwa huo kwa miaka miwili mfululizo hadi wagonjwa wanne waliporipotiwa kwenye jimbo la Borno mwei Julai na Agosti mwaka 2016.

WHO kupitia makala maalum iliyotolewa hii leo ambayo ni siku ya kutokomeza Polio duniani, imesema visa hivyo vilipatikana Borno ambako ni eneo lisilo na usalama, lakini kwingineko miundombinu ya utoaji chanjo iko thabiti na inafanya kazi.

“Kufuatia kubainika kwa polio huko Borno, serikali ilitangaza kuwa mlipuko  huo ni dharura ya kiafya ya kitaifa, tangazo lililofuatiwa na kampeni kubwa ya utoaji chanjo. Kisa cha mwisho cha polio Nigeria kiliripotiwa tarehe 27 Septemba mwaka 2016,” imesema WHO.

 

Mkunga awapa chanjo dhidi ya polio Mama na mtoto wake mchanga.
Photo: UNICEF/Prashanth Vishwanathan
Mkunga awapa chanjo dhidi ya polio Mama na mtoto wake mchanga.

 

Dkt. Dkt Halima Isa ambaye ni afisa afya anatambuliwa kwa ubobezi wake kwenye utoaji chanjo dhidi ya polio, na ni mmoja wa kikundi cha watoa chanjo, wasimamizi, viongozi wa kijamii, wasimamizi ngazi ya kata, mamlaka za mitaa na zile za serikali kuu.

Mifumo ya kuzuia Polio yasaidia kukabiliana na milipuko ya magonjwa

 WHO inasema mifumo hiyo iliyowekwa wakati huo inatumiwa pia  hata sasa kukabiliana na milipuko ya kipindupindu katika majimbo ya Adamwa, Bauchi, Borno, Gombe na Yobe.

Kamishna wa afya katika jimbo la Bauchi Dkt. Zuwaira Ibrahim Hassan anasema timu hizo za utoaji chanjo ndio mabingwa wa afya kwenye jamii zao wakati wa kuelimisha jamii kuhusu athari za maambukizi ya ugonjwa huo na kwamba “katika masuala ya kukabiliana na kipindupindu, watendaji hawa wa polio kwa kawaida wanapita nyumba kwa nyumba kusaka wagonjwa, kuelimisha jamii kuhusu afya na njia za kujikinga pamoja na kutoa chanjo dhidi ya kipindupindu.”

 

Afisa wa afya akitoa chanjo ya matone dhidi ya polio kwa mtoto.
UNICEF/UN018102/Al-Khatib
Afisa wa afya akitoa chanjo ya matone dhidi ya polio kwa mtoto.

 

Akizungumzia mfumo huo, mwakilishi wa WHO nchini Nigeria Dkt. Wondimagegnehu Alemu amesema, “miundombinu dhidi ya Polio nchini Nigeria inahusisha mfumo ulioendelezwa mno ambao serikali na wadau wanaweza kutumia ili kufanikisha lengo la kuwa na afya kwa wote.”

Ameongeza kuwa “tutaendelea kufanya kazi pamoja na serikali kuu na serikali za majimbo ili kufanikisha usimamizi wenye mafanikio kwenye janga hilo la kipindupindu na pia kwenye milipuko mingine kwa kutumia makundi ya watoa huduma walio mstari wa mbele kwenye jamii.”

Baadhi ya harakati zinazofanywa wakati wa mlipuko wa polio ni kama vile kukusanya takwimu za wagonjwa, kuzichanganua, kutoa taarifa na pia kuhifadhi wakitumia simu za mkononi.

Maafisa wa WHO Nigeria wanakisifia kikosi cha kupambana na kwa mchango wake ambao ulisaidia kukabiliana na mlipuko wa homa ya Lassa mapema mwaka 2018.  

 Polio ni nini?

 Polio ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vinavyoshambulia mishipa ya fahamu na hivyo kusababisha mtu kupooza na hata kifo.

WHO inasema polio hadi sasa haina tiba bali ina kinga ambayo ni chanjo.

Shirika hilo la afya duniani linasema katika miaka ya 1980, ugonjwa huo ulikuwa ukiathiri takribani watu 350,000 katika nchi 125 kila mwaka.

Juhudi za kuangamiza polio zilianza mwaka 1988 na tangu hapo idadi ya maambukizi imepungua kwa asilimia 99 na sasa polio imebaki Afghanistan , Pakistan na Nigeria.