Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bila takwimu sahihi, ajenda 2030 itasalia ndoto- Bi. Mohammed

Takwimu sahihi ni muhimu ili kuweza kubaini jinsi ya kushughulikia majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi. Kama katika picha mtu akirusha ndege isiyo na rubani kupata data sahihi za uharibifu huko Ufilipino
©FAO/Veejay Villafranca
Takwimu sahihi ni muhimu ili kuweza kubaini jinsi ya kushughulikia majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi. Kama katika picha mtu akirusha ndege isiyo na rubani kupata data sahihi za uharibifu huko Ufilipino

Bila takwimu sahihi, ajenda 2030 itasalia ndoto- Bi. Mohammed

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mkutano wa kimataifa kuhusu takwimu umeanza leo huko Dubai, Falme za Kiarabu ambapo Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed amesema mafanikio ya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs yanategemea uwepo wa takwimu sahihi na za kutosha.

Akihutubia washiriki, Bi. Mohammed amesema kwa kuwa na takwimu sahihi, jumuishi, zinazowakilisha kila jinsi na kila upande na pia zilizonyambuliwa vya kutosha, serikali zinaweza kuelewa changamoto ambazo zinakabili dunia hivi sasa na kubainisha suluhisho sahihi kwa changamoto hizo.

Ametolea mfano takwimu kuhusu kujiandaa dhidi ya majanga na mifumo ya kutoa onyo mapema, takwimu ambazo amesema zinaweza kusaidia kuokoa maisha pindi majanga yanapotokea.

“Mwaka jana pekee majanga yalisababisha dunia kupoteza jumla ya dola bilioni 330,” amesema Bi. Mohammed akitolea mfano Mexico ambayo kwa kutambua athari za majanga imeweka mfumo wa kutoa onyo na kwamba tangu mwaka 1993 imetoa maonyo 158 na hivyo kupunguza athari za majanga.

Naibu Katibu Mkuu amesema kwa kuwa na takwimu sahihi, “wanafunzi wanaweza kupata fursa za ajira na wanawake wanaweza kujifunza sheria zinazowalinda dhidi ya ubaguzi. Ina maana raia wanaweza kufuatilia pia utendaji wa serikali zao na kuwajibisha watunga sera na viongozi wa serikali.

Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed
IISD/ENB | Kiara Worth
Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed

Amesema pindi raia wanapokuwa na uwezo wa kufanya hivyo, imani kwa serikali yao inaongezeka na hivyo kufungua fursa mpya.

Kwa mantiki hiyo Naibu Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema jukumu sasa ni kuhakikisha watu wanapata takwimu na kwamba zinatumika kufanikisha utekelezaji wa ajenda 2030 katika ngazi zote na maeneo yote ya dunia.

“Ndio maana Umoja wa Mataifa unaongoza juhudi za  kimataifa za kujumuisha takwimu na mifumo ya taarifa. Kanzi data wazi kwa ajili ya maendeleo endelevu inaruhusu amtaifa kuleta pamoja vyanzo mbalimbali vya takwimu kwa ajili ya kuhakikisha uamuzi unaofanyika unazingatia takwimu sahihi na pia uchechemuzi,” amesema Bi. Mohammed.

Amegusia wavuti ya viashiria vya SDG akisema inapatia fursa watu wanaoitumia kuona simulizi na takwimu kuhusu utekelezaji wa SDGs, hivyo amesihi serikali ziwekeze katika utafutaji wa takwimu sahihi kwa maendeleo na uwezeshaji wa jamii kuanzia ngazi ya taifa hadi vijijini.