Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yapongeza wanawake viongozi Afrika kwa kuweka mjadala wa vizazi tofauti

Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed
IISD/ENB | Kiara Worth
Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed

UN yapongeza wanawake viongozi Afrika kwa kuweka mjadala wa vizazi tofauti

Wanawake

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J.Mohammed ameshiriki mkutano wa mtandao wa wanawake viongozi barani Afrika, AWLN, akipongeza mtandao huo kwa kuchuuka hatua za kuleta pamoja viongozi wanawake wastaafu, wale wa sasa na viongozi vijana.

Bi. Mohammed amesema mtandao huo unaonesha njia ya kwamba, “tunaweza kuvuka tofauti za umri na kuunganisha wanawake, hususan wanawake wa Afrika na kwa pamoja kushughulikia changamoto za dunia zinazotuathiri sote, iwe ni ukosefu wa usawa wa jinsia, maendeleo endelevu, ghasia au haki kwenye tabianchi.”

Miongoni mwa wanawake viongozi walioshiriki ni Rais wa zamani wa Malawi Joyce Banda, Rais wa zamani wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf pamoja na Rais wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Catherine Samba-Panza pamoja na viongozi vijana ambao nao walipata fursa ya kuzungumza katika mkutano huo wa siku tatu ulioanza jana tarehe 16 na utamalizika kesho jumapili mjini Nairobi, Kenya.

Katika hotuba yake, Bi. Mohammed amezungumzia kuletwa pamoja kwa wanawake wa vizazi viwili tofauti na kusema kuwa, “kuna  umuhimmu wa mazungumzo kati ya vizazi hivi, kama mkutano huu ili kusisitiza maadili yetu ya pamoja ikiwemo umuhimu wa kutomwacha yeyote nyuma, kusongesha utofauti, stahamala na jamii zisizo na mizozo.”

Halikadhalika amesema mashauriano kama hayo yanasaidia kuchagiza urithi wa kiafrika na utambulisho wa kiafrika akisema kuwa, “natiwa moyo kuona vijana hawa kimkakati kabisa wakisongesha malengo hayo, ikiwemo kuhoji mifumo iliyopo, kupanga mambo mapya na kutumia vyema teknolojia. Na ninaamini kuwa tunaweza kujifunza mno kutoka kila mmoja wet una kunufaika na uzoefu wetu wa uongozi .”

Mikutano ya ngazi ya juu Septemba New York

Naibu Katibu Mkuu akakumbushia pia mikutao ya ngazi ya juu itakayofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mwezi ujao wa Septemba ikiwemo wa mabadiliko ya tabianchi, huduma ya afya kwa wote, tathmini ya malengo ya maendeleo endelevu, ufadhili kwa maendeleo na ule wa nchi za visiwa vidogo.

Usawa wa jinsia

Bi.Mohammed amegusia pia athari hasi za ukosefu wa usawa wa jinsia barani Afrika akisema kuwa hugharimu takribani dola bilioni 95 nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara kila mwaka.

“Afrika imeweka mwelekeo katika miaka ya karibuni, lakini bado haiko katika kufanikisha malengo yake kwa mujibu wa ajenda yake ya 2063. Malengo hayo ni pamoja na asilimia 50 ya wanawake kwenye ofisi za kuchaguliwe katika ngazi ya serikali kuu, kanda na mitaa pamoja na asilimia 50 kwenye nafasi za uongozi,” amesema Bi. Mohammed.

Alice Senna Philip, mwenyekiti wa kikundi cha wanawake jimboni Yei nchini Sudan Kusini akizungumza mbele ya ujumbe wa ngazi ya juu wa UNMISS ulioongozwa na mkuu wao David Shearer. Ujumbe huo ulitembelea eneo hilo.
UNMISS/Francesca Mold
Alice Senna Philip, mwenyekiti wa kikundi cha wanawake jimboni Yei nchini Sudan Kusini akizungumza mbele ya ujumbe wa ngazi ya juu wa UNMISS ulioongozwa na mkuu wao David Shearer. Ujumbe huo ulitembelea eneo hilo.

Halikadhalika amesema ukosefu wa usawa wa jinsia unagharimu amani endelevu barani Afrika. “Kuanzia kaskazini mwa Nigeria hadi Sudan, wanawake wakiwemo wasichana wanachukua dhima nzito za kuzuia mizozo na kuchagiza amani. Lakini pale mazungumzo yanapokuwa rasmi, au kipindi cha mpito kinapofika, wanaenguliwa na sauti zao zinazimwa na michango yao inakandamizwa.”

Amesema hii haipaswi kuachwa iendelee na labda tunaweza kuchukua Sudan kama mfano wa kwanza ambako wanawake walihoji mfumo uliopo na kuleta mabadiliko na wanawake ndio wapitisha maamuzi.

Ushirikiano wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika

Je uwepo wa Naibu Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa kwenye mkutano huo ni kiashiria gani cha uhusiano kati ya Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika? Ni swali ambapo Newton Kanema wa kituo cha habari za Umoja wa Mataifa, UNIC Nairobi alimuuliza Bi. Mohammed kando ya mkutano huo ambapo Bi. Mohammed amesema, “hakika na ni muhimu sana kwa kuwa kwa muda mrefu katika Muungano wa Afrika tulifanikiwa kuwa na usawa wa jinsia kwenye uongozi wa kamisheni zake na sasa tuna usawa wa jinsia kwenye uongozi wa juu na kile tunachotaka kusema kama wanawake ni kwamba tupo hapa kwa sababu tuna uwezo wa kutekeleza majukumu tunayopatiwa.”

Amesema kuwa, “ kile tunataka kufanya ni kuimarisha zaidi uhusiano na na kuona sawa wa jinsia na idadi sawa ya uongozi kama jambo endelevu si jambo la mara moja na kupita. Na ni kweli hii ni sehemu ya kuimarisha ubia ambao mwenyekiti wa kamisheni ya AU Mahammat Faki na Katibu Mkuu Antonio Guterres wako makini kuona unafanya kazi.”

Naibu Katibu Mkuu amesema pia wamezindua mfuko wa wanawake ambao ni kwa ajili ya wale wanaosimamia mafungu ya fedha za uwekezaji, “kwa hiyo ni mwelekeo mwingine kabisa si tu kwa ajili ya kujitolea bali kuwezesha watu wachukue jukumu la kusimamia fedha na kuweka usawa kwa wanwake wafanyabiashara.”

Akiwa mjini Nairobi, Kenya, Naibu Katibu Mkuu amekuwa pia na mazungumzo na viongozi na wafanyakazi wa ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini humo, UNON.