Kampeni za uchaguzi wa Rais Afghanistan ziwe huru- UNAMA

29 Julai 2019

Wakati kampeni za uchaguzi wa rais nchini Afghanistan zikiwa zimeanza jana Jumapili Julai 28 hadi tarehe 25 mwezi ujao wa Septemba, Umoja wa Mataifa umesihi wagombea na wafuasi wao wahakikishe kampeni zinakuwa huru na zinafuata kanuni za sheria ya uchaguzi.

Taarifa ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, UNAMA iliyotolewa leo kwenye mji mkuu Kabul, imetaka pia wagombea na wafuasi wao wazigatie kanuni za uchaguzi kwa mujibu wa tume ya huru ya taifa ya  uchaguzi pamoja na kanuni nyingine zilizopitiwa na tume hiyo.

“Wadau wote lazima wajenge imani katika mchakato mzima wa uchaguzi na inatumainiwa kuwa kampeni zote zitapatia fursa wananchi wa Afghanistan taarifa za kutosha kuweza kuweza kutekeleza haki yao ya kuchagua kiongozi wanaomtaka,” imesema taarifa ya UNAMA.

Halikadhalika UNAMA imesema kuwa vyombo vya habari navyo vina jukumu muhimu katika mchakato wa uchaguzi, na kwamba “kama ilivyo kwa wananchi, vyombo hivyo navyo vihakikishe vinatekeleza dhima yao kwa kuweka mazingira sawa na ya amani wakati wa kipindi cha kampeni.”

Ujumbe huo umesihi wapiga kura waliojiandikisha washiriki kwenye  uchaguzi huo, ikiwemo wanawake kama njia mojawapo ya kuelekeza utashi wao wa kidemokrasia.

Sambamba na hilo UNAMA imesema vyama vyote vinapaswa kutambua wajibu wao kisheria ikiwemo agizo la raia kwa watumishi wa umma kutoingilia mchakato mzima wa uchaguzi sambamba na vikosi vya usalama.

“Maafisa wote wa serikali kisheria wanapaswa kutenganisha majukumu yao ya kiserikali na kampeni za uchaguzi au wasitekeleza mambo ambayo yatakuwa na manufaa kwa wagombea mahsusi,” imesema taarifa hiyo ya UNAMA.

UNAMA kwa upande wake inasisitiza kuwa itaendelea kutekeleza ahadi yake ya kusaidia mchakato utakaoongozwa na wananchi wenyewe wa Afghanistanna inatambua juhudi za vyombo vya  uchaguzi, serikali na wadau wengine katika kuhakikisha uchaguzi wa rais unafanyika kwa wakati, kwa uwazi na unakuwa halali.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud