Shambulizi saa 48 kabla ya uchaguzi Afghanistan lazusha hofu:UNAMA

19 Oktoba 2018

Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan UNAMA, umelaani vikali shambuzi la jana Alhamisi dhidi ya ofisi za serikali mjini Kandahar na kusema muda wa shambulizi hilo ambao ni saa 48 tu kabla ya uchaguzi wa bunge umechangia kueneza hofu na taharuki ya usalama wakati raia wengi wakijiandaa kutekeleza haki yao ya kikatiba ya kuchagua wawakilishi wao.

UNAMA imesema imetambua uamuzi wa serikali ya Afghanistan kuahirisha uchaguzi wa bunge kwenye jimbo la Kandahar kwa wiki moja na itaendelea kushirikiana na taasisi husika ili kuhakikisha kwamba watu wa Kandahar watachagua wawakilishi wao kwa mujibu wa haki yao ya kikatiba.

UNAMA pia imetiwa moyo na hatua zilizochukuliwa na serikali za kudumisha utulivu na serikali kuendelea kufanya kazi japo katika mazingira magumu.

UNAMA imetuma salamu za rambirambi kwa familia na jamaa wa waliopoteza maisha katika shambulio hilo na kuwatakia nafuuu ya haraka majeruhi.

Duru zimasema miongoni mwa waliouawa katika shambulio hilo la risasi ni kamanda wa polisi wa Kandahar, jenerali Abdul Raziq na mkuu wa upelelezi wa jimbo hilo Jenerali Abdul Momin . Kundi la kigaidi la Taliban limedai kuhusika na shambulio hilo.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter