Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kimbunga Luban chaacha maafa Yemen:OCHA

Familia iliyopoteza makazi ikiwa imejiegesha kwenye Hema nchini Yemen
OCHA/Giles
Familia iliyopoteza makazi ikiwa imejiegesha kwenye Hema nchini Yemen

Kimbunga Luban chaacha maafa Yemen:OCHA

Msaada wa Kibinadamu

Eneo lililoathirika zaidi ni jimbo la Al Maharah na kuna hofu kwamba mvua zinazoendelea kunyesha zinaweza kusababisha mafuriko zaidi. Kwa mujibu wa OCHA, tathimini ya awali inaonyesha kuwa kaya zaidi ya 3,000 zimetawanywa na mafuriko hayo, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka wakati tathimini ya kina itakapoweza kufanywa katika maeneo yote yaliyoathirika.

Wakazi 550 wamefanikiwa kupata makazi ya muda katika shule moja kwenye wilaya ya Ghaydah baada ya kupoteza makazi kwenye mafuriko hayo na wadau wa misaada ya kibinadamu wanaendelea kuwasaidia ikiwemo kuwapa vifaa vya malazi, huduma za afya na kuisaidia hospitali kubwa ya Ghaydah kutoa huduma zinazohitajika.

OCHA inasema ndege mbili zilizotumwa na Saudia zimewasili kwenye uwanja wa ndege wa Ghaydah Oktoba 17 zikiwa na shehena ya tani 440 za chakula kutoka kituo cha msaada cha mfalme Salman na tani zingine 125 za vikapu vya chakula zimesafirishwa kwa malori hadi mpkanani kwa saudia.

Mtoto wa umri wa miaka 12 akiwa amebeba sabuni alizopatiwa na UN nchini Yemen
OCHA/Muath Algabal
Mtoto wa umri wa miaka 12 akiwa amebeba sabuni alizopatiwa na UN nchini Yemen

 

Msaada pia unatolewa na mashirika yasiyo ya kiserikali yaani NGO’s. Hatahivyo uharibifu uliyosababishwa na kimbunga hicho unazuia barabara kupitika katika baadhi ya wilaya zilizoathirika na daraja kubwa linalounganisha majimbo ya Al Maharah na Hadramaut limeharibiwa vibaya na hivyo kulazimu mashirika ya misaada kusaka njia mbadala ili kuweza kuwafikia waathirika wa wilaya hizo wanaohitaji msaada wa haraka.