Dola bilioni 2.6 zaahidiwa kuinusuru Yemen:UN

26 Februari 2019

Wahisani waliokusanyika mjini Geneva  Uswisi hii leo wameahidi dola bilioni 2.6 ili kuhakikisha kwamba operesheni za misaada ya kibinadamu zinaendelea nchini Yemen katika wakati huu ambao msaada ndio tumaini pekee la mamilioni ya Wayemen. 

Kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA, ahadi hizo katika mkutano wa kimataifa wa uchangishaji fedha kwa ajili ya Yemen  ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na ahadi ya dola bilioni 2.1 iliyotolewa mwaka jana ambayo ilitimizwa kwa asilimia 100.  Wahisani 16 wameongeza ahadi zao mwaka huu zikiwemo Falme za nchi za Kiarabu UAE, Uingereza, Muungano wa Ulaya, Ujerumani na Canada.

Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo Mkuu wa OCHA Mark Lowcock amesema vita vinavyoendelea vinawabebesha gharama kubwa hususn wanawake na watoto nchini Yemen, wakiwemo watoto 360,000 walio na utapiamlo uliokithiri. Ameongeza kuwa lakini wanawake hawa na wasichana pia wanaweza kuwa ni sehemu ya suluhu

“Moja ya vitu tunavyofanya katika mpango wetu wa misaada ya kibinadamu kwa mwaka huu ni kuunda mkakati ambao wanawake na wasichana watashiriki kama sehemu ya suluhu. Na ninawachagiza wakati mkitoa ahadi zenu kufikiria njia ambazo mtatusaidia kufanikisha hili.”

WFP/Marco Frattini
Katika kituo cha afya cha uzazi Al Sabeen Sana'a Yemen, WFP inatoa lishe iliorutubishwa kutibu mtoto Ali Yakya Ali anayeugua utapiamolo uliokithiti wakati babake akifuatilia. Novemba 2018

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza umuhimu wa amani ya kudumu katika mkutano huo amesema,

“Ingawa bado kuna safari ndefu , viunzi vingi vya kuruka , lakini kuna ishara ya matumaini. Ninazitaka pande zote kuendelea na majadiliano na kuchagua njia ya amani ya kudumu, Mshikamano wa jumuiya ya kimataifa na uungaji mkono wan chi wanachama katika mchakato wa amani umekuwa na utaendelea kuwa muhimu.”

Mpango wa usaidizi wa kibinadamu wa Yemen kwa mwaka 2019 unahitaji dola bilioni 4 ili kuwafikia watu milioni 21.4 ambao wanahitaji msaada haraka huku nusu ya fedha hizo zitaelekezwa katika msaada wa dharura wa chakula kwa watu milioni 12 idadi yao ikiwa ni ongezeko la asilimia hamsini ikilinganishwa na mwaka 2018.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud