Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

De Mistura naye 'kuachia ngazi' mzozo wa Syria mwezi Novemba, asema ni kwa sababu za kibinafsi

Staffan de Mistura, Mjumbe maalum wa UN kwa Syria wakati kikao cha Baraza la Usalama kuhusu hali ya Mashariki ya Kati hii leo Oktoba 17, 2018
UN /Rick Bajornas
Staffan de Mistura, Mjumbe maalum wa UN kwa Syria wakati kikao cha Baraza la Usalama kuhusu hali ya Mashariki ya Kati hii leo Oktoba 17, 2018

De Mistura naye 'kuachia ngazi' mzozo wa Syria mwezi Novemba, asema ni kwa sababu za kibinafsi

Amani na Usalama

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, Staffan de Mistura ametumia hotuba yake kwa wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo jijini New York, Marekani kutangaza mambo makuu mawili ikiwemo kualikwa kwake huko Damascus, Syria kwa ajili ya mchakato wa mazungumzo na kung’atuka wadhifa huo mwezi ujao wa Novemba.

Akizungumzia mwaliko huo kutoka serikali ya Syria, Bwana de Mistura amesema ni mwendelezo wa mkutano wao na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati wa mjadala mkuu wa Baraza Kuu la umoja huo.

Amesema atatua fursa hiyo ya wiki ijayo kushirikisha serikali ya Syria juu ya kazi iliyofanyika ya kuunda kamati ya katiba na kwamba, “nitakuwa tayari, bila shaka iwapo Baraza hili litapenda, niwapatie taarifa baada ya ziara yangu iwapo mashauriano haya ya uso kwa uso yamezaa matunda kama tunavyotarajia kuhusu uridhiaji na kukubaliwa kwa orodha ya tatu ya watakaokuwemo kwenye kamati hiyo ya kikatiba, orodha ambayo ni halali na jumuishi.”

Kamati hiyo ya kikatiba inapaswa kuwa na orodha tatu, ambapo orodha ya kwanza ni ya upande wa serikali ya Syria, orodha ya pili ni  upande wa upinzani na orodha ya tatu ni ya watu wasiofungamana na upande wowote ambayo imeandaliwa na Umoja wa Mataifa.

Sasa maeneo mengi ya Syria kwenye mji wa Aleppo yamesalia mahame kutokana na mapigano yaliyosababisha maelfu ya wananchi kukimbia mji huo
UNHCR/Susan Schulman
Sasa maeneo mengi ya Syria kwenye mji wa Aleppo yamesalia mahame kutokana na mapigano yaliyosababisha maelfu ya wananchi kukimbia mji huo

Mjumbe huyo maalum amesema ni matarajio yake kuwa atakuwa katika nafasi ya kutuma mwaliko kwa wahusika ili aitishe kikao cha kamati ya kikatiba mwezi ujao akisema “siwezi kutabiri iwapo inawezakana au la lakini ninachofahamu ni kwamba baada ya miezi 9 ya maandalizi ni vyema kuzindua kamati halali ya kikatiba na chochote kitakachotokea ningalipenda kurejea hapa na kuwaarifu.”

Na ndipo akazungumzia hatua yake ya kung’atuka nafasi hiyo akisema, “ mimi mwenyewe nitaondoka wiki  ya mwisho ya mwezi Novemba. Nimepata heshima kubwa kuhudumu kwa miaka minne na miezi minne kama mjumbe maalum. Kwa muda mrefu nimekuwa najadiliana na Katibu Mkuu juu ya nia yangu ya kung’atuka kwa sababu za kibinafsi. Nimeshukuru sana kwa kitendo chenu cha kuniunga mkono wakati wa kipindi chote.”

Akizungumzia mpango huo wa de Mistura kung’atuka nafasi hiyo, Katibu Mkuu Antonio Guterres amemshukuru kwa mchango wake wa dhati wa kusongesha mbele mchakato wa amani Syria, nchi ambayo imekumbwa na mzozo tangu mwezi Machi mwaka 2011.

Tayari Katibu Mkuu kupitia msemaji wake amesema ataanzisha mchakato wa kumpata mrithi wa de Mistura.

Wengine waliowahi kushika wadhifa huo hayati Kofi Annan ambaye aling’atuka mwaka 2012 na nafasi yake kuchukuliwa na Lakhdar Brahimi ambaye naye pia alijiuzulu mwaka 2014.

Lakhdar Brahimi naye aliwahi kuongoza mchakato wa amani Syria na kujiuzulu
UN/Eskinder Debebe
Lakhdar Brahimi naye aliwahi kuongoza mchakato wa amani Syria na kujiuzulu