Niko tayari kwenda Idlib kuwasaidia raia:De Mistura

30 Agosti 2018

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mgogoro wa Syria anasema yuko tayari kwenda Idlib kusaidia kuhakikisha usalama wa raia walio katikati ya hofu ya mashambulizi yanayotarajiwa kufanywa na serikali.

Ongezeko la operesheni za majeshi ya serikali ya Syria yanayokusudia kurejesha eneo la Idlib kunaweza kusababisha athari kubwa, amesema leo mwakilishi huo Staffan de Mistura .

Akizungumza na wanahabari mjini Geneva, Bwana De Mistura alijitolea yeye mwenyewe kuwasindikiza wakazi wa Idlib hadi katika maeneo salama kabla ya shambulizi lolote katika eneo pekee lililosalia likishikiliwa na wapinzani nchini humo, ikikumbusha ahadi kama hiyo aliyoitoa pia mwaka 2016 kwa ajili ya Aleppo.

Maoni hayo ya de Mistura yanarejelea wito wa awali wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ambaye alitahadharisha dhidi ya operesheni ya kijeshi na kuelezea hofu yake juu ya hatari ya kutokea ‘janga la binadamu’

SAUTI YA STAFFAN DE MISTURA 

“Hakuna Idlib nyingine, wanaweza kwenda wapi?. “Mtu anaweza kwenda wapi?” Kwa hivyo kila wakati kulipokuwa na hatari na kukawa na hatima ya mgogoro huo, kulikuwa na mahali ambako mtu angechagua kwenda. Hakuna Idlib nyingine” 

 

UN Photo/Violaine Martin
Staffan de Mistura, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria.

 

Hatima ya Idlib ni muhimu kwa sababu wakazi wake wengi wamepoteza makazi yao au wamehamishwa kutoka katika maeneo mengine yenye vita kabla ya maeneo hayo kurejea katika vikosi vya serikali kwenye vita hivyo vya zaidi ya miaka saba.

De Mistura ameongeza kwamba Idlib ni eneo la mwisho nchini Syria ambalo lina makubaliano ya kusitisha vita, akikumbushia makubaliano kati ya Urusi, Uturuki na Iran wakifahamika kama”wadhamini wa  Astana” baada ya mji huo mkuu wa Kazakhstan kutumika kama eneo ambako makubaliano yalifikiwa. Hivyo amehoji

SAUTI YA STAFFAN DE MISTURA

“Kwa nini haraka ya kiasi hicho na kusiwe na muda zaidi wa kuruhusu majadiliano zaidi hususani miongoni mwa wadhamini wa Astana”

Katika miezi sita pekee iliripotiwa kuwa watu laki tano walifika Idlib baada ya kukimbia machafuko  katika mji wa Dera’a Ghouta Mashariki  na maeneo mengine yanayodhibitiwa na wapinzani.

 

Jimbo la kaskazini magharibi pia ni ‘ngome ya wapiganaji wa kigeni’, amesema Bwana de Mistura akifafanua kuwa wapiganaji wa Al Nusra au Al Qaeda ambao wanatambuliwa na Umoja wa Mataifa kama magaidi waliongezeka na  kufikia takribani elfu kumi .

Wapiganaji hao  wanafahamika kuwa na uwezo wa matumizi ya silaha za kemikali  za chlorine kama ilivyo serikali ya Syria, amesema Bwana de Mistura akisisitiza uwezekano wa kutokea kwa janga kubwa wakati wa shambulizi la kijeshi.

Ingawa hakuna anayehoji haki ya Serikali ya Syria kupambana na hao waliotambuliwa na Umoja wa Mataifa kuwa ni magaidi, au haki ya Syria kurejesha maeneo yake, hakukuwa  na sababu ya kutumia silaha nzito katika maeneo yanayokaliwa na watu wengi,..

Akirejerea tamko la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alilolitoa Jumatano, amesema matumizi ya silaha zisizoweza kudhibitiwa katika makazi yenye watu wengi yanaweza kuwa ni uhalifu wa kivita.

Ameongeza kuwa litakuwa jambo la ajabu mwishoni mwa vita ndani ya Syria kukiwa na mauaji ya kutisha yanayohusisha watu wengi kabla ya kujitolea kwenda Idrib.

 

© UNICEF/UNI150195/Diffidenti
Mvulana huyu akipita maeneo yaliyoharibiwa kufuatia mashambulizi nchini Syria.

 

Aliwahi nia yake ya kutaka kufanya hivyo kwa Aleppo mwaka 2016 ilikataliwa na Al Nusra, na amewakumbusha wanahabari akisema kuwa hali hiyo ilisababisha maelfu ya watu kupoteza maisha.

SAUTI YA STAFFAN DE MISTURA

“Kwa hivyo kwa mara nyingine tena nimejiandaa, kushiriki mimi mwenyewe safari hii kwa kushirikiana na serikali kwa sababu hilo ni eneo ambalo wanalidhibiti nje ya Idlib”. Kuhakikisha fursa ya muda inapatikana kwa ajili ya watu kupita na kuweza kurejea kwenye maeneo yao bila kuguswa mara baada ya hili kukamilika”

Akijibu maswali, afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema hana maelezo maalumu kuwa shambulizi mjini Idlib linakaribia. “Lakini nina taarifa kuhusu maandalizi, ujumbe na maelezo” . “Na kwa kuwa bado tunazungumza, wawili kati ya wadhamini wakuu, katika suala hili Uturuki na Urusi wanajali na nina matumaini tutafanikiwa katika kukwepa janga kubwa”

Juhudi za Umoja wa Mataifa kupata suluhisho la amani kwa vita vya Syria zimepangwa kuendelea na kukiwa na mikutano iliyopangwa kufanyika mjini Geneva tarehe 10 na 11 mwezi Septemba ikihusisha wawakilishi kutoka Urusi, Uturuki na Irani.

Majadiliano hayo yanategemewa kufuatiwa tarahe 14 na mikutano juu ya masuala ya Katiba ikihusisha viongozi wa ngazi ya juu kutoka katika nchi nyingine saba wanachama ikiwamo Misri, Ufaransa, Ujerumani, Jordan, Saudi Arabia, Uingereza na Marekani.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud