Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabadiliko ya katiba Syria yatatanabaisha mbivu na mbichi:De Mistura

Mapigano Kusini Magharibi mwa Syria yanweka hatarini maisha ya watu 750,000 wengi wakiwa ni watoto, kama hawa pichani  waliokimbia Deraa.
UNICEF/Al-Faqir
Mapigano Kusini Magharibi mwa Syria yanweka hatarini maisha ya watu 750,000 wengi wakiwa ni watoto, kama hawa pichani waliokimbia Deraa.

Mabadiliko ya katiba Syria yatatanabaisha mbivu na mbichi:De Mistura

Amani na Usalama

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya  Syria, Staffan de Mistura, amesema anatarajia kukutana na maafisa wa ngazi ya juu wa Urusi, Uturuki na Iran mnamo Septemba 10 na 11 , katika majadiliano ya muendelezo wa mikutano iliyofanyika Geneva na Sochi hapo awali.

 

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva Uswisi,  de Mistura amesema kuunda kamati ya kusimamia mabadiliko ya katiba Syria ndio mtihani

“Kamati ya katiba inaweza kuwa na inapaswa kuwa ndio mlango sasa wa kuingilia kwenye kile tunachokiita mchakato wa kuaminika wa kisiasa endapo tu kamati hiyo itakuwa ya kuaminika pia.” 

Amesema hata hivyo hawezi na hatotabiri leo kwamba mchakato utafika wapi wakikutana tarehe 10 na 11 mwezi huu.

”Lakini naweza kusema yafuatayo, utakuwa ni wakati muhimu wa kujua ukweli, pili orodha hii ya tatu ya wapinzani wa serikali kama tunavyoiita, wameshirikishwa na wako tayari kwa mkutano tarehe 10 na 11 na wamekuwepo hapo kwa muda mrefu. Hivyo pia chaguo muhimu ni jinsi gani ya kusaidia upande wa Syria kuandaa kazi ya kamati ya katiba.”

 Ameongeza kuwa wanatumai hakutokuwa na tukio litakaloingilia au kuvuruga mipango hiyo, ingawa ameweka wazi kwamba “kama mnavyofahamu dhoruba kubwa haisababishwi na upepo, bali na siasa na binadamu, hivyo tunahitaji kuliangalia suala hili katika pande zote kisiasa na kiufundi.”

Wakati huohuo mashirika ya masuala ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa yanaripoti kuwa kumekuwa na mashambulizi kadhaa ya anga katika eneo la Idlib Magharibi na Kaskazini mwa eneo la vijijini la Hama, na kusababisha vifo na majeruhi , pia uharibifu wa miundombinu ya raia zikiwemo shule na soko. Takriban watu milioni wanakisiwa kuwepo Idlib.