Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

   Mgogoro wa kibinadamu Syria si wa kwisha leo wala kesho:Al-Zaatar

Mtoto akiwa ameketi kwenye dawati ndani ya moja ya darasa la shule iliyoshambulia huko Idleb nchini Syria mwaka 2016
UNICEF
Mtoto akiwa ameketi kwenye dawati ndani ya moja ya darasa la shule iliyoshambulia huko Idleb nchini Syria mwaka 2016

   Mgogoro wa kibinadamu Syria si wa kwisha leo wala kesho:Al-Zaatar

Amani na Usalama

Mgogoro wa kibinadamu nchini Syria ni mkubwa, hauishi leo wala kesho na watu wanaohitaji msaada ni takriban milioni 13. Kauli hiyo imetolewa na mratibu mkazi na mkuu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Syria , Ali Al-Za’tari alipozungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani hii leo.

Bwana Al-Za'tari ameongeza kuwa fikra hiyo ni kutokana na hali halisi ambayo imeghubikwa na wimbi kubwa la wakimbizi nje na ndani, ukosefu wa huduma za msingi na huku watu wengine wakiendelea kufungasha virago kila siku katika maeneo yanayokabiliwa na mapigano kama Ghouta Mashariki .

(SAUTI YA ALI AL-ZA’TARI)

“Hatudhani kama mgogoro wa kibinadamu nchini Syria utamalizika mwaka 2019, pengine utaendelea hadi mwaka 2020 na miaka mingine ijayo. Tuna wakimbizi wa ndani milioni 6.2 Syria, wakiwa zaidi katika maeneo ya Alepo, jimbo la Damascus vijijini na Idlib.

Bwana Al-Za’tari amesema mwaka huu pekee kumekuwa na watu takriban milioni 1.2 waliohama makwao wengi wakiwa ni wanawake na watoto. Idadi hii ikimaanisha  kuna watu ambao wamelazimika kuhama zaidi ya mara moja kwa mwaka huu.

 

Mapigano Kusini Magharibi mwa Syria yanaweka hatarini maisha ya watu  wengi wakiwa ni watoto, kama hawa pichani  waliokimbia Deraa.
UNICEF/Al-Faqir
Mapigano Kusini Magharibi mwa Syria yanaweka hatarini maisha ya watu wengi wakiwa ni watoto, kama hawa pichani waliokimbia Deraa.

Kwa sasa kuna mashirika zaidi ya 14 ya Umoja wa Mataifa yanatoa huduma mbalimbali nchini Syria yakiwa na makao mjini Damascus na yamefanikiwa kuendesha opereshi zake kila kona ya nchi hiyo isipokuwa Idlib, na changamoto kubwa ni fedha za kutosha kukidhi mahitaji ya mamilioni ya wanaohitaji msaada

(SAUTI YA ALI AL-ZA’TARI)

“Tuko katika utekelezaji wa mpango wa usaidizi wa kibinadamu wa mwaka 2018, ambapo tuliomba dola bilioni 3.4 kwa ajili ya Syria, na tumeshapokea asilimia 45 sawa na dola bilioni 1.5. Hofu yetu hivi sasa ni kutuvusha hadi 2019, msaada wetu ni wa kutokana na mahitaji,  hivyo tunahitaji kuwalenga wale wanaohitaji msaada wa kibinadamu”

Ameongeza kuwa ili  kufanikisha hilo tathimini ya mahitaji ya ulinzi, afa, elimu, maji na usafi,  chakula, na masuala mengine ya msingi inahitajika , na hii inamaanisha “tupatiwe fursa ya kuweza kufika kila mahali kwa uhuru kufanya tathimini hiyo na kutoa tarifa itakayosaidia kuusanya rasilimali za kutosha kukidhi mahitaji yote hayo.”

Amesema vita vya Syria ambavyo viko mwaka wa saba vinahitaji mshikamano wa kimataifa ili kuvikomesha na kuwaondolea madhila raia wa nchi hiyo ambayo wengine wamepoteza kila kitu ikiwemo uhai wa wapendwa wao.