Nitatumia vikao vya wiki ijayo kuchagiza ushirikiano wa kimataifa unaopigwa vita: Guterrres

20 Septemba 2018

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amesema ingawa ushirikiano wa kimataifa unakumbwa na zahma, yeyé binafsi bado anaamini ndio njia sahihi ya kutatua matatizo yanayokumba dunia wakati huu wa utandawazi.

Katibu Mkuu ameyasema  hayo leo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani alipozungumza na waandishi habari ikiwa ni katika kuelekea kuanza kwa vikao vya ngazi ya juu wiki ijayo vikileta pamoja marais 84 na wakuu wa serikali 44.

Bwana Guterres bila kufafanua kwa kina, amesema ushirikiano wa kimataifa unalaumiwa sana hivi sasa lakini amesema ana mpango aliouita ni madhubuti kwa lengo la kushughulikia changamoto dhidi ya ushirikiano wa kimataifa.

Nitatumia mikutano yangu  pamoja na nafasi zingine wiki ijayo  ili kushinikiza kurejelewa upya kwa mfumo wa kimataifa unaozingatia kanuni na pia Umoja wa Mataifa. Umoja wa Mataifa ni jukwaa muhimu  kwa ushirikiano  wa  kimataifa. Kuwepo kwa  marais 84 na wakuu wa serikali 44 ni ishara tosha  ya imani  ya jamii ya kimataifa waliyonayo kwa Umoja wa Mataifa.”

Katika mkutano huo amegusia pia masuala ya amani na usalama ikiwemo zahma inayoendelea huko Idlib nchini Syria ambako raia wanakumbwa na mashambulizi kiholela.

Kwa mantiki hiyo Bwana Guterres amewapongeza marais wa Uturuki na Urusi, mataifa ambayo yamejihusisha moja kwa moja na mgogoro huo, kwa kufikia mkataba wa  kuweka eneo huru lisilo la mapigano sehemu za Idlib nchini Syria na kuwataka watekeleze yale walioyokubaliana.

 “ Ikiwa utatekelezwa sawasawa, utawaondolea zahma  raia wa kawaida  miliioni 3 pamoja na  watoto milioni 1.”

Pia amegusia mgogoro wa Yemen akisema kuwa raia  wa kawaida wanaendelea kuteseka  na vita nchini humo kutokana sio tu na mashambulizi ya angani yanayofanywa na vikosi vya ushirika pamoja na vikosi vya ardhini vya pande zote husika, lakini pia na  hatua ya vikosi vya wahouthi kuendelea kuvurumisha makombora  nchini Saudi Arabia.

Ameomba  pande zote na wafuasi wao kujizuia  dhidi ya hatua ambayo zinaweza kuchochea mapigano zaidi. 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter