Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tafadhali majeshi ya serikali Syria msishambulie Idlib: Guterres

Msichana wa umri wa miaka saba asimama mbele ya jengo la shule lililoharibiwa  mjini Idlib Syria.
UNICEF
Msichana wa umri wa miaka saba asimama mbele ya jengo la shule lililoharibiwa mjini Idlib Syria.

Tafadhali majeshi ya serikali Syria msishambulie Idlib: Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka serikali ya Syria na washirika wake wapige moyo konde na waachane na mipango yao ya kushambulia zaidi eneo la Idlib nchini Syria.

Bwana Guterres amesema hayo leo jijini New York, Marekani alipozungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliokuwa mahsusi kwa suala la Idlib eneo ambalo amesema halipaswi kugeuzwa uwanja wa vita.

 "Ni jambo muhimu kuepusha mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya Idlib na ikiwa litatokea litasababisha zahma ya kibinadamu ambayo haijaonekana  katika mgororo wenye umwagikaji mwingi wa damu nchini Syria.”

Katibu Mkuu amesema Idlib ni eneo ambalo limekuwa kimbilio la watu wengi wa Syria wakiwemo watoto wapatao milioni moja na kwa kuwa ni kimbilio la wengi lisigeuzwe uwanja wa umwagaji damu.

Na ndipo Bwana Guterres akatoa wito kwa washirika au watu na nchi zilizo na uhusiano wa karibu na Syria

'Nasihi pande zote zinazohusika moja kwa moja au kwa njia nyingine, hususan wadhamani watatu wa ukanda usio na mapigano ambao ni Iran, Urusi na Uturuki; tumieni jitihada zenu zote kusaka suluhu ambayo inalinda raia. Lindeni huduma za msingi kama vile hospitali. Hakikisheni mnaheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu.”

Wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa unakuja kukiwa na taarifa kuwa serikali ya Syria ikisaidiana na  Urusi inapanga mashambulio makali dhidi ya Idlib ili kuwafurusha wapiganaji wanaoipinga serikali kutoka Idlib, eneo ambalo yadaiwa kuwa ni ngome ya mwisho inayoshikiliwa na wapiganaji hao.

Katibu Mkuu amerejelea tena kauli yake ya kwamba hakuna suluhu yoyote ya mzozo wa Syria zaidi ya mazungumzo na kwamba suluhu ya kijeshi haiwezi kuleta chochote zaidi ya machungu.

 

Martins Griffiths, Mjumbe Malalum wa UN kuhusu Yemen, akilihutubia baraza la Usalama la Umataifa 11 Septemba 2018 kutoka Amman Jordan.
UN Photo/Loey Felipe
Martins Griffiths, Mjumbe Malalum wa UN kuhusu Yemen, akilihutubia baraza la Usalama la Umataifa 11 Septemba 2018 kutoka Amman Jordan.

 

Katika hatua nyingine mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen Martin Griffiths, amehutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuelezea changamoto za juhudi zake  za kupatanisha makundi yanayopigana ili kuweza kuokoa maisha ya raia.

Akizungumza kupitia Video kutoka Geneva Uswisi mjumbe huyo maalum kuhusu Yemen amesema kuwa  mapigano nchini humo yanazidi kuongezeka, pande husika hazijakutana kwa kipindi cha zaidi ya miaka  miwili, kiwango cha matumaini kiko chini na athari za kibinadamu pamoja na madhara kwa wanadamu vinaongezeka.

Ameongeza kuwa wakati pande kinzani  zikiwa zimejikita  katika makabiliano ya ghasia , waathirika wakuu wa vita hivyo, watu wa Yemen, wanahaha kwa suluhu ya kisiasa ambayo itawaondolea mateso, kumaliza vita  na pia kuwapa serikali itakayoshughulikia  mahitaji yao muhimu.

Bwana Griffiths ameliarifu Baraza hilo kuwa baada ya miezi kadhaa ya mashauriano na makundi husika, mazungumzo ya Geneva yalianza,  ingawa hayakwenda kama ilivyopangwa , bado ameweza kuzindua tena mchakato wa kisiasa kwa kuungwa mkono na watu sio tu wa Yemen lakini pia na jamii ya kimataifa.