Korea Kaskazini na Korea Kusini, sasa ni wakati wa vitendo halisi-Guterres

20 Septemba 2018

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres amekaribisha matokeo yaliyofikiwa kwenye mkutaon wa tatu wa mwaka kati ya viongozi wa Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK na Jamhuri ya Korea ijulikanayo pia kama Korea Kusini.

Mazungumzo hayo ya Jumatano kati ya Rais Kim Jong Un wa Korea Kaskazini na Moon Jae-in wa Korea Kusini yalifanyika mjini Pyongyang, Korea Kaskazini kwa lengo la kuimarisha amani na kuepusha silaha za nyuklia katika rasi ya Korea.

Makubaliano kati ya pande hizo yaliyoko kwenye taarifa ya pamoja yanajumuisha kujenga uhusiano wa kuaminiana kati ya majeshi ya pande zote mbili na ahadi ya Korea kaskazini kuharibu mitambo yake ya nyuklia mbele ya watalaamu kutoka katika nchi zinazohusika.

Kupitia msemaji wake, Katibu Mkuu Guterres amepongeza mipango na diplomasia ambayo imefanikisha makubaliano muhimu yaliyoko katika azimio la pamoja lililofikiwa hii leo mjini Pyongyang akisema, “sasa ni wakati wa vitendo halisi.”

Katibu Mkuu ametoa wito wa kuungana kwa jumuiya ya kimataifa kuunga mkono pande hizi mbili katika mpango wao kuelekea amani endelevu, usalama na uangamizaji wa mitambo ya nyuklia katika rasi ya Korea kulingana na maazimio ya Baraza la Usalama. 

Aidha Katibu Mkuu amekumbushia juu ya utayari wa mfumo wa Umoja wa Mataifa kusaidia pande zote kwa kila njia itakayoonekana inafaa.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud