Baraza la Usalama lataka suluhu ya kisiasa kwa mzozo rasi ya Korea

30 Novemba 2017

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao kuhusu harakati za kutokomeza silaha za nyuklia huku hoja ya Korea Kaskazini kufanya jaribio la kombora la masafa marefu usiku wa kuamkia leo ikipatiwa kipaumbele.

Mkuu wa Idara ya Siasa kwenye Umoja wa Mataifa Jeffrey Feltman alihutubia kikao hicho kilichohudhuriwa pia na mwakilishi wa kudumu wa Korea Kaskazini kwenye Umoja wa Mataifa ambapo alirejelea kauli ya Katibu Mkuu Antonio Guterres aliyotoa baada ya kombora hilo kurushwa.

Bwana Feltman alianza hotuba yake kwa kunukuu shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini na vyanzo vingien vya habari vya nchi hiyo vikieleza kuwa tarehe 29 mwezi huu saa nane na dakika 48 usiku kwa saa za Korea Kaskazini, nchi hiyo ilirusha kombora la masafa marefu lililotua eneo la kipekee la kiuchumi kwenye bahari ya Japan.

(Sauti ya Jeffrey Feltman)

“Hii ni mara ya 13 Baraza hili linakutana mwaka huu wa 2017. Kitendo cha Korea Kaskazini kurejea mara kwa mara na majaribio ya nyuklia na makombora kwa kipindi cha miaka miwili kimeongeza mvutano kwenye rasi ya Korea na kwingineko. Mwenendo huu lazima ubadilishwe. “

image
Mwakilishi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Nikki Haley na Mwakilishi kutoka Ujumbe wa Kudumu wa Korea Kusini  kwenye Umoja wa Mataifa wakizungumza kabla ya kuanza kwa kikao. (Picha: UN/Rick Bajornas)

Hata hivyo Bwana Feltman amesema suluhu ya kisiasa ndio muarobaini wa mvutano unaoendelea hivi sasa kwenye rasi ya Korea huku akisema kuwa..(Sauti ya Jeffrey Feltman)

“Kwa kuzingatia hatari zinazohusiana na hatua za kijeshi, Baraza la Usalama katika kutekeleza wajibu wake wa msingi lichukue kila hatua ili kuzuia hatari zaidi. Umoja ndani ya Baraza la Usalama ni muhimu. Umoja huo utaweka fursa ya kuendeleza mashauriano ya kidiplomasia, fursa ambayo inapaswa kutumiwa katika mazingira ya sasa hatari ili kuweka mazingira bora ya mazungumzo.”

Baadhi ya wajumbe waliochangia mjadala huo ambao haukuhudhuriwa na Korea Kaskazini au DPRK, wamerejelea wito kwa Korea Kaskazini ijulikanayo pia kama Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK iachane na mwenendo huo kwani unatishia usalama na amani duniani.

Mathalani wametaka nchi ziendelee kuzingatia vikwazo dhidi ya DPRK ikiwemo biashara na nchi hiyo.

image
Wawakilishi wa China na Urusi wakijadili jambo kabla ya kuanza kwa kikao cha Baraza la Usalama. (picha:UN/Rick Bajornas)

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud