Mabadiliko ya tabianchi kuathiri sekta za kilimo na mifugo- FAO

17 Septemba 2018

Mabadiliko ya tabianchi yataathiri uzalishaji katika sekta ya kilimo na mifumo ya biashara ya kimataifa, imesema ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya masoko ya mazao ya kilimo duniani.

Ikiwa imetolewa leo na shirika la chakula na kilimo duniani, FAO ripoti hiyo inaangazia zaidi uhusiano kati ya biashara ya mazao ya kilimo, mabadiliko ya tabianchi na uhakika wa chakula.

Mathalani ripoti inasema ifikapo katikati mwa karne hii viwango vya wastani vya joto, kubadilika kwa kiwango cha unyevunyevu, ongezeko la viwango vya maji ya bahari, na matukio ya hali ya hewa ya kupindukia pamoja na uwezekano wa uharibifu wa mazao kutokana na wadudu na magonjwa vinatarajiwa kuwa na madhara kwenye uzalishaji wa mazao, mifugo, uvuvi na kilimo cha mazao ya baharini.

UNICEF/Mukwazhi
Ukame unazidi kuathiri ardhi ya sehemu kubwa katika bara la Afrika.

Hata hivyo ripoti inaeleza kuwa kilimo cha kimataifa kinatoa fursa ya kushughulikia changamoto hiyo sambamba na biashara ya kimataifa kwa kuwa chakula cha ziada kinaweza kuuziwa nchi ambazo zinakabiliwa na uhaba kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa FAO Jose Graziano da Silva amesema ni wazi kuwa nchi zinazoendelea ikiwemo zile za Afrika zitahitaji msaada kutoka nchi tajiri ili zitekeleze mipango ya kuhimili na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na hatimaye mifumo ya kilimo na chakula iwe endelevu.

FAO
Ripoti ya UN kuhusu hali ya masoko ya bidhaa za kilimo, ripoti ambayo imezinduliwa leo

Bwana da Silva amesema hatua nyingine ni kutunga na kutekeleza sera ambazo zinabadili mfumo wa kimataifa wa uzalishaji kwenye kilimo uwe endelevu zaidi na kulinda nchi na maeneo yaliyo hatarini zaidi kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi.

Amesema na wakati huo huo kurahisisha mfumo wa biashara ili hatimaye ufanikishe lengo namba 2 la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs na hiyo itakuwa jambo muhimu iwapo itashuhudiwa ulimwenguni bila njaa na utapiamlo ifikapo mwaka 2030.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud